HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 20, 2017

WAZIRI NAPE AUNDA KAMATI KWA AJILI YA KUCHUNGUZA TUKIO LA UVAMIZI WA KITUO CHA HABARI CHA CLOUDS

Na Shamimu Nyaki-WHUSM

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye ameunda kamati ya watu watano itayoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dkt.Hassan Abbas kuchunguza tukio la uvamizi lilofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda katika chombo cha habari cha Clouds Media.

Akiongea katika ziara aliyoifanya  leo  Jijini Dar es Salaam  katika chombo hicho Mhe.Nape amesema Kamati hiyo itafanya kazi ndani ya masaa 24 kuanzia sasa huku akiwataja wajumbe wengine  kuwa ni Bw. Frank Balile,Bibi.Johanes Neng’ida,Bw.Jessy Kwayu na Bibi. Mabel Mabisa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Serikalini (TCRA).

“Kamati hii ipo kwa ajili ya kupata maelezo ya kutosha kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw.Paul Makonda ili tuwe na taarifa iliyokamilika na kujua hatua itakayofuata” alisema Mhe.Nape.

Aidha Waziri Nape ameeleza kuwa kitendo cha uvamizi kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa kipo kinyume na Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kwa kuwa sheria hiyo ipo kwa ajili ya kulinda wanatasnia hao.

Aliongeza na kufafanua kuwa Serikali imesikitishwa na kitendo hicho na ndio maaana akaunda kamati ya uchunguzi itakayokuja na taarifa kamili huku akiwataka wanatasnia ya habari na wananchi kuwa watulivu na kusubiri majibu ya uchunguzi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Habari ya Clouds Bw.Joseph Kusaga amemshukuru Waziri Nape kwa kuonyesha ushirikiano na kuwa pamoja katika jambo hilo huku akifurahishwa na namna Serikali inavyowajali wadau wa Habari.  

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) Bw.Reginald Mengi amempongeza Mhe. Waziri kwa hatua ya kuunda kamati ya uchunguzi  kwakuaanaamini itatoa matokeo chanya yatakayolinda heshima ya Tasnia ya Habari nchini.

 “Uamuzi wa kuunda kamati hii ni jambo la hekima na busara linaloendana na misingi ya taaluma ya habari nasi tutakuwa radhi kuunga mkono hatua  zitachukuliwa katika kulinda uhuru wa habari nchini” alisema Bw.Mengi.


Tukio la kuvamiwa kwa kituo cha Clouds Media Group na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Paul Mkonda   limetokea usiku wa  Machi 17 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages