HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 14, 2017

Waziri Nape awataka Maafisa Mawasiliano Serikalini kutendea haki Sheria ya Huduma za Habari na Sheria ya Haki ya kupata Taarifa

Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO Dkt Hassan Abbas akichangia jambo wakati  wa kikao cha 12 cha Maafisa Mawasiliano  wa Serikali kinachofanyika Mkoani Dodoma.
 Maafisa Mawasiliano wa Serikali kutoka Wizara,Taasisi, Halmashauri,Wakala na Mashirika ya Umma,Tamisemi na Idara zinazojitegemea wakimskiliza kwa makini Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye (hayupo Pichani)  wakati akifungua Kikao kazi  cha 12 cha Maafisa hao kinachofanyika Mkoani Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi Bi.Elizabeth Kitundu akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao kazi cha 12 cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali kinachofanyika Mkoani Dodoma. 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bi.Nuru Milao akiongea kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye kufungua rasmi  Kikao kazi  cha 12 cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali kinachofanyika Mkoani Dodoma tarehe 14 Machi 2017. 
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye akizungumza na Maafisa Mawasiliano wa Serikali wakati akifungua kikao kazi  cha 12 cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali kinachofanyika Mkoani Dodoma. 

Mwenyekiti  wa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) akichangia jambo wakati wa Kikao kazi cha 12 cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali kinachofanyika Mkoani Dodoma. 
 Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye akiwa katika picha ya pamoja na wadhamini wa Kikao kazi cha 12 cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali kinachofanyika Mkoani Dodoma.Kulia  kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi.Nuru Milao,Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi Bi.Elizabeth Kitundu,Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dkt.Hassana Abbas na Mwenyekiti  wa TAGCO Bw.Innocent Mungy.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Nnauye akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Mawasiliano kutoka Idara ya Habari-MAELEZO wakati wa kikao cha 12 cha Maafisa hao wa Serikali kinachofanyika Mkoani Dodoma. Kulia  kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi.Nuru Milao,Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi Bi.Elizabeth Kitundu,Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dkt.Hassana Abbas na Mwenyekiti  wa TAGCO Bw.Innocent Mungy.

Na: Lorietha Laurence – WHUSM, Dodoma

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye amewataka Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kuzisoma, kuzielewa na kuzifanyia kazi sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na ile ya Haki ya kupata Taarifa  ya mwaka 2016 ili kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kuuhabarisha umma.

Waziri Nape ameyasema hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa akifungua mkutano wa Maafisa Mawasiliano Serikalini ambapo licha ya kuwataka kuzijua sheria hizo pia amewataka kuwa wabunifu kuendana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika utendaji kazi wa kila siku.

Aidha aliongeza kuwa kuwepo kwa sheria hizo mbili kutatengeneza daraja litakalounganisha na kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa wananchi.

Ni wajibu wa Maafisa Mawasiliano kuzijua na kuzitendea kazi sheria hizi ili kurahisisha upatikanaji wa mawasiliano baina ya serikalini na umma hivyo kuondoa ugumu uliokuwepo hususani katika kupatikana kwa taarifa muhimu kwa wananchi alisema Waziri Nape.

Aliongeza kwa kufafanua kuwa endapo utekelezaji wa sheria hizi mbili muhimu utasimamiwa na kuzingatiwa basi kutakuwepo na matokeo chanya ya kiutendaji na hivyo kuleta mafanikio makubwa yanayotarajiwa na umma.

Waziri Nape pia aliwataka Maafisa Mawasiliano hao kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuendana na maendeleo ya teknolojia ikiwemo matumizi ya mitandao ya kijamii katika kuhabarisha umma na kutoa taarifa kwa wakati.

Zama hizi sio zile za maafisa mawasiliano kujisifia kwa kuwa na safari nyingi badala yake kuwa watekelezaji wa kazi zao kwa wakati na matokeo yanayoonekana kwa umma ila kwa atakayeshindwa kutekeleza hayo basi tutaomba atupishealisema Waziri Nape.

Aidha alieleza kuwa anafahamu kuwa kuna changamoto nyingi ambazo maafisa mawasiliano wanakumbana nazo katika utendaji wao wa kazi ikiwemo ukosefu wa vifaa ingawa si kigezo cha wao kutokutekeleza wajibu wao.

Katika kuhakikisha kuwa changamoto ya ukosefu wa vifaa inatatuliwa Waziri Nape alitoa Wito kwa Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuweka kipaumbele katika bajeti hii mpya kwa kutenga kiasi cha fedha ambacho kitasaidia kununua vifaa kwa ajili ya Maafisa Mawasiliano wa Wizara, Taasisi, Mikoa, Wilaya na Halmashauri.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao alisema kuwa umuhimu wa mkutano wa Maafisa Mawasiliano Serikalini ni katika kuwajengea uwezo wa kiutendaji pamoja na kutathmini utendaji kazi wao.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Elizabeth Simon Kitundu ameishukuru Wizara kuandaa mafunzo kwa Maafisa Mawasiliano Serikalini na kuyafanyia Mkoani Dodoma kwani kwa kufanya hivyo itarahishisha mfumo wa kimawasiliano na kutangaza fursa zilizopo Mkoani Dodoma hivyo kuwafanya watumishi wa umma kuwa na amani katika kutekeleza agizo la kuhamia Dodoma.

Mkutano wa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini umefanyika kwa mara ya 12 huku lengo ikiwa ni kuwakutanisha kwa pamoja maafisa hao kutoka katika ngazi mbalimbali za kiutendaji serikalini ikiwemo Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa, Wilaya na Halmashauri ili kuweza kubadilishana uzoefu wa kiutendaji pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment

Pages