HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 26, 2017

WORLD CROSS COUNTRY 2017

Ni zamu ya Tanzania medali?
NA TULLO CHAMBO, KAMPALA
 LEO macho na masikio takribani duniani kote yataelekezwa jijini hapa, pale kati ya matukio makubwa katika mchezo wa riadha dunia lkitakapofanyika, nalo si jingine bali ni mbio za Nyika ‘IAAF World Cross Country’ zitakaporindima.

Tanzania ikiwa kati ya nchi zaidi ya 150 wanachama wa Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), tayari kikosi chake cha wanariadha 28 kiko jijini hapa tangu juzi usiku tayari kwa kinyang’anyiro hicho kitakachopigwa viwanja vya Kololo.

Mara baada ya kuwasili juzi usiku kwa usafiri wa basi maalumu lililotolewa na Jeshi la Kujenga la Taifa (JKT), huku ikifadhiliwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), na kufikia hoteli ya Africana, kilipata mapokezi mazuri kutoka kwa Ubalozi wa Tanzania jijini hapa.

Jana asubuhi, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Maleko Nderimo akiambatana na Mwambata, Brigedia Jenerali S. Makona, walifika kuzungumza na wachezaji na kuwapa hamasa ili leo wafanye kweli.

Balozi Nderimo, aliwataka kuweka woga wa majina pembeni na kuhakikisha leo wanaipeperusha vema bendera ya Tanzania.

Aliwataka kutanguliza nidhamu ya kimichezo na kuonyesha ushindani wa hali ya juu na kwamba kwenye nia pana njia na pia watambue wamekuja kushindana na si kushindwa.

Kwa upande wake Meneja wa Timu ya Tanzania, Metta Petro, alieleza kuwa hali ya timu ni nzuri isipokuwa mchezo mmoja alikuwa na homa lakini afya yake imeimarika na leo atacheza.

Aidha, aliwakumbusha wosia walioachiwa na Rais wa Shirikisho la Riadha la Tanzania (RT), Anthony Mtaka, wakati akiwakabidhi bendera ya Taifa, kuhakikisha wanampa raha Rais John Magufuli siku ya kesho Jumapili.

Naye Meneja Uhusiano wa TANAPA, Paschal Shelutete, aliwatakia kila la heri wachezaji na kuwataka wasiwaangushe mamilioni ya Watanzania walioko nyuma yao.

Baadhi ya nyota wanaotarajiwa kupeperusha vema bendera ya Tanzania leo mbele ya mataifa yenye rekodi kali katika medani ya riadha duniani kama Kenya, Ethiopia na mengineyo niEmmanuel Giniki, Bazil John, Gabriel Geay, Fabiano Joseph huku kwa wanawake ni  Magdalena Crispin, Angelina Tsere, Failuna Abdi, Sara Ramadhani, Jackline Sakilu na wengineo.

No comments:

Post a Comment

Pages