HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 20, 2017

KATIBU MKUU WIZARA YA MAJI NA UMWAGILIAJI PROF. KITILA MKUMBO ARIDHISHWA NA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA MAJISAFI

Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo (Kushoto) akionyeshwa na Mkandarasi wa Kampuni ya WABAG toka nchini India maeneo ambayo maji yanapita kuelekea kwa wananchi wakati wa ziara yake ya kikazi katika eneo la tanki la maji safi lililopo Kibamba 19 Aprili, 2017.

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiaji Prof. Kitila Mkumbo leo ametembelea Mtambo wa Ruvu Juu uliopo eneo la Mlandizi Mkoani Pwani na kujionea kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kupitia Wizara anayoiongoza.    
Akiwa mtamboni hapo alipata fursa ya kushuhudia mtambo huo ukifanya kazi kama ilivyotarajiwa baada ya upanuzi wake kukamilika, ambapo hivi sasa mtambo una uwezo wa kuzalisha maji safi na salama kiasi cha lita milioni 196 kwa siku. 

Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara yake Mkoani hapo, Prof. Kitila amesema kwamba ziara hiyo ni muhimu kwake kwa kuwa amejifunza mambo mengi kuhusu namna maji yanavyopatikana ambapo ametoa pongezi kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika eneo hilo.

“Uwekezaji huu ni mkubwa sana uliofanyika katika eneo hili, uwekezaji huu unahitaji kutunzawa ili kudhibti upotevu wa maji”, alisema Prof. Mkumbo.
Amewataka Mameneja wa Miradi ya Maji kuhakikisha kuwa wanajiwekea malengo katika kuwahudumia wananchi na ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha kwamba wanayatunza maji wayapatayo kwakuwa upatikanaji wake ni mrefu na Serikali imewekeza fedha nyingi katika kuyapata maji hayo.

Aidha, Serikali imetekeleza mradi huo kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) ambapo katika ziara yake hiyo ameweza kupita na kujionea maeneo mbalimbali yanayozalisha maji na kuyahifadhi ikiwemo Matenki ya maji yaliyopo eneo la Chuo Kikuu cha Ardhi yenye ujazo wa lita milioni 45, tenki la maji safi la Kibamba lenye ujazo wa lita milioni 10, Ruvu Darajani (In-take), Mtambo mpya wa Ruvu Juu.

Sambamba na ziara hiyo, Prof. Kitila alipata wasaa wa kutembelea Ofisi ya Dawasco iliyopo Kibaha na kuktana na watendaji wa ofisi hiyo akiwemo Meneja wa DAWASCO Kibaha, Bw. Erasto Mbwambo ambaye alitoa taarifa yake kuhusu maendeleo yaliyofikiwa katika kuhakikisha kuwa maji yanawafikia wananchi jambo ambalo lilimfurahisha Prof. Kitila.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) Bw. Romanus Mwangingo ameeleza kuwa, kwa sasa tayari maji toka Mtambo wa Ruvu Juu yameanza kuzalishwa baada ya shughuli za upanuzi katika mtambo huo kakamilika.

Ziara hiyo iliandaliwa na Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) na kuhudhuriwa na Maofisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, DAWASA, DAWASCO, Wakandarasi pamoja na Mshauri wa mradi wa mfumo wa maji wa Ruvu Juu.

No comments:

Post a Comment

Pages