HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 07, 2017

Kocha wa kuogelea kutoka uingereza avutiwa na vipaji vya Tanzania

 Aravind Raghavendran wa Bluefins akishindana katika mashindano ya Taifa.
 Celina Itatiro akishindana katika mashindano ya taifa.
 Collins Saliboko anayesoma Uingereza akishindana katika mashindano hayo
Kocha Sue Purchase kutoka shule ya St Felix y Ungereza akijadiliaja jambo na viongozi wa TSA 
Sonia Tumioto wa DSC na pia anayesoma Uingereza akishindana katika mashindano hayo. 
waogeleaji wakichupa 'divi' wakati wa mashindano ya Taifa kwenye bwawa la hopac.

Na Mwandishi Wetu

Kocha maarufu wa mchezo wa kuogelea  Uingereza, Sue Purchase amevutiwa na vipaji vilivyonyeshwa na waogeleaji wengi chipukizi huku akitoa wito kwa wadau kushirikiana chama cha kuogelea (TSA) kuondoa changamoto mbalimbali.

Purchase alisema hayo  wakati wa mashindano ya klabu bingwa ya Tanzania  yanayoendelea kwenye bwawa la shule ya Hopac na kudhaminiwa na Davis & Shirtliff, CRDB Bank, Mediterraneo Hotel & Restaurant, Coca Cola, Aggrey & Clifford  na The Terrace.

Amesema kuwa  kuna waogeleaji wengi wa Tanzania ambao wanaweza kufanya vyema katika mashindano ya kimataifa, lakini tatizo kubwa ni vifaa hasa bwawa la kuogelea la viwango vya kimataifa ambalo hakuna nchini.

“Kwa kweli nimefarijika sana, nimeona waogeleaji wengi wenye vipaji ambao kama wataendelezwa, nchi inaweza kufanya vyema katika mashindano ya kimataifa hasa Jumuiya ya Madola, Dunia na Olimpiki ya 2020 mjini Tokyo, Japan,”

“Kinachotakiwa sasa ni kubadili mfumo wa mazoezi kwa kutumia vifaa vilivyopo,  waogeleaji wengi  wanaonekana kuchoka kwa muda mfupi kutokana na kukosa muda wa kutosha wa mazoezi, ili kufikia viwango, wanahitaji kuongeza muda wa kufanya mazoezi,” alisema Purchase.

Alifafanua kuwa ni vigumu kufanya vyema kimataifa kwa kufanya mazoezi kwa masaa mawili au matatu na jioni tu wakati waogeleaji wan chi nyingine wanafanya mazoezi asubuhi na jioni kwa masaa mengi zaidi.

Mweyekiti wa Kamati ya Ufundi ya TSA, Amina Mfaume amekiri kuwa tatizo kubwa ni muda wa mazoezi na kusema hiyo inatokana na kubanwa kwa waogeleaji na shughuli za masomo.

“Ni kweli kuwa waogeleaji wetu hawapati muda muafaka wa mazoezi, kuna tatizo la shule na vifaa,  timu nyingi zinafanya mazoezi kwenye mabwawa ya shule na lazima wafanye hivyo jioni baada ya muda wa masomo,”

“Pia kuna suala la gharama za kukodi bwawa ambazo ni kubwa sana, hivyo klabu nyingi zinalipia gharama kutokana na muda usiozidi uwezo wa kifedha,” alisema Amina.

Katibu Mkuu wa TSA, Ramadhani Namkoveka alisema kuwa wanajitahidi kutafuta wadau ili kusaidia ujenzi wa mabwawa ya kisasa ya kuogelea ili kuwawezesha waogeleaji wengi kupata muda zaidi wa mazoezi kwa gharama nafuu.

Jumla ya waogeleaji 172 kutoka klabu 15 nchini zimeshiriki katika mashindano hayo ambayo yanamalizika Jumamosi jioni ambapo washindi watatangazwa.

No comments:

Post a Comment

Pages