HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 24, 2017

VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUHIMIZA NIDHAMU-MAJALIWA


Kamishina Jenerali wa  Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya, Nchini, Rogers Siyanga akizungumza katika Kongamano kuhusu Mmonyoko wa Maadili lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na kufunguliwa na Waziri Mkuu, kassim Majliwa kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius, kambarage Nyerere jijini Dar es salaam Aprili 24, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Alhaji  Abubakary Zuberi akizungumza katika Kongamano kuhusu Mmonyoko wa Maadili lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na kufunguliwa na Waziri Mkuu, kassim Majliwa kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius, kambarage Nyerere jijini Dar es salaam Aprili 24, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemani Jafo akizungumza katika Kongamano kuhusu Mmonyoko wa Maadili lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na kufunguliwa na Waziri Mkuu, kassim Majliwa kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius, kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Kongamano kuhusu Mmonyoko wa Maadili lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Kongamano kuhusu Mmonyoko wa Maadili lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)  kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius, kambarage Nyerere jijini Dar es salaam.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini nchini kutumia nafasi zao kuhimiza wazazi na walezi kuishi maisha yenye nidhamu, kuthamini kazi yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu na kusimamia malezi ya watoto na kuzingatia maadili ya Taifa kwa ujumla.
Tabia na mwenendo mzuri ni lazima uanzie katika ngazi ya familia, mtaani na hatimaye katika jamii. Tukirudia utamaduni wetu wa zamani wa kusimamia maadili kwa pamoja, jamii yetu itanusurika kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Aprili 24,2017) wakati akifungua kongamano kuhusu mmomonyoko wa maadili na athari za dawa za kulevya lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, lililofanyika mjini Dar es Salaam.

Amesema kila mzazi au mlezi aone aibu, uchungu na ajutie anapoona mtoto yoyote akienda kinyume na utaratibu wa kawaida wa maisha na ni vema wakatumia nafasi yao kwa kuwahimiza vijana hao waishi maisha ya nidhamu na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu.
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga jamii yenye  kuzingatia maadili nchini na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli amekuwa akiwasisitizia Watanzania wote kuzingatia maadili katika jamii kwa kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vyote vya rushwa na ubadhirifu.
Amesema maadili katika Taifa ni moja ya tunu muhimu kwa kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha maendeleo, ujenzi wa umoja, amani, upendo, uvumilivu na mshikamano kwa jamii.
Amesema maadili ni nyenzo muhimu sana katika ujenzi wa Taifa na huliepusha kuingia katika mifarakano na migogoro. “Hivyo hatuna budi nasi kuyalinda maadili hayo kwa uwezo wetu wote, ili tuyarithishe kwa vizazi vijavyo, kama vile sisi tulivyoyarithi kutoka kwa waasisi wa Taifa letu,”.
“Hata hivyo, ninyi ni mashahidi kuwa katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia vitendo vya mmomonyoko wa maadili na matokeo yake yanaonekana dhahiri kama kuongezeka kwa vitendo vya rushwa, kuiga tamaduni za nchi za kigeni ambazo sio njema na hazina tija kwa jamii, na Taifa kwa ujumla”.
“Ni ukweli usiopingika kuwa mmomonyoko wa maadili ni miongoni mwa vichocheo vinavyopelekea matumizi ya dawa haramu za kulevya. Hivyo ni matarajio yangu kuwa mtaliangalia kwa kina tatizo la mmomonyoko wa maadili ambalo kwa kiasi kikubwa linatuathiri kama Taifa katika mipango ya Serikali na maendeleo ya Taifa letu,” amesema.

Hivyo Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa BAKWATA kwa kuwa na wazo la kufanya kongamano hilo lenye kulenga kujadili namna ya kurejesha maadili katika jamii. Tukumbuke kuwa Watanzania tutaendelea kuishi kwa upendo, amani na utulivu iwapo tutazingatia maadili.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo mstari wa mbele kuhakikisha kuwa mapambano na vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inafanikiwa. Lengo ni kuhakikisha kuwa waathirika wote wa matumizi ya dawa hizo wakiwemo vijana, ambao ndio nguvu kazi ya Taifa wanakombolewa dhidi ya janga hilo.
Amesema Serikali itahakikisha inashughulikia mtandao wa wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na dawa za kulevya bila ajizi, ambapo vyombo vyote vya kisheria vimeelekezwa kushirikiana katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa ya kulevya kwa kusimamia sheria ipasavyo.
Naye Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Bw. Rogers Siyanga amewaomba viongozi wa dini kuiunga mkono mamlaka hiyo kwa sababu inafanya kazi kubwa ambayo inahitaji msaada wa watu wote.
Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Alhaji Abubakary Zuberi amesema viongozi wa dini nchini wana jukumu la kukataza maovu na kuiamrisha jamii kufanya mambo mema badala ya kuiachia Serikali pekee kufanya kazi hiyo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, APRILI 24, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages