HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 09, 2017

Waimbaji mguu sawa Tamasha la Pasaka

NA MWANDISHI WETU
ZIKISALIA siku sita kabla ya kishindo cha Tamasha la muziki wa injili la Pasaka litakalofanyika katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, waimbaji wote wapo katika maandalizi ya mwisho kabla ya tukio.
Tamasha hilo la kimataifa litakalozinduliwa Uwanja wa Uhuru mbele ya mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, litafika pia Simiyu na Mwanza.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusu maandalizi ya tukio hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Alex Msama alisema kila kitu kinakwenda vizuri na waimbaji wote wapo katika maandalizi.
“Nashukuru kwa upande wetu Kamati mipango inakwenda vizuri kama ilivyopangwa. Kama unavyojua, Pasaka ilionekana kama vile iko mbali sana, lakini siku zimefika,” alisema Msama.
Alisema anashukuru pia waimbaji wote watakaohudumu katika tamsha la mwaka huu, wapo vizuri na wanaendelea na maandalizi ya mwisho kuelekea kishindo cha Jumapili katika Uwanja wa Uhuru.
Msama ametoa wito kwa wadau wa muziki wa injili kulipokea tukio hilo kwa mikono miwili kupata Baraka za Mungu kupitia tukio hilo lenye hadhi ya kimataifa litakalowaleta waimbaji wa ndani na nje ya nchi.
Alisema kwa kutambua kiu ya wengi kutaka kulishuhudia Tamasha hilo, ndio maana wameweka viingilio vya kawaida kuanzia sh 10,000 kwa viti maalumu, sh 5000 kwa wakubwa na watoto sh 3,000.
Msama alisema baada ya kutoka Uwanja wa Uhuru, uhondo wa tukio hilo utahamia mkoa wa Simiyu hapo April 22 na siku itakayofuata, itakuwa zamu ya wakazi wa jiji la Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba.
Waimbaji ambao watapamba tukio hilo ni mwimbaji wa kimataifa wa Afrika Kusini, Solly Mahlangu, Mercy Masika na Danny ‘M’ na Faustine Munishi  kutoka Kenya.
Kwa upande wa kwaya, ni Ulyankuru maarufu kama Kwa Viumbe Vyote, Kinondoni Revival Choir itakayozindua kazi yao mpya isemayo ‘Ngome Zimeanguka’ na Vijana KKKT Tabata, jijini Dar es Salaam.
Waimbaji ni Rose Muhando atakayezindua albamu yake ya Jitenge na Ruth, Jesca BM, Upendo Kilahiro, Matha Mwaipaja, Christina Shusho, John Lissu na Boniface Mwaitege.

No comments:

Post a Comment

Pages