HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 28, 2017

Wakazi wa Manispaa ya Musoma Mjini Wadaiwa Mil. 271 za Kodi ya Ardhi

Na Husna Saidi- MAELEZO

Takribani shilingi milioni 271 zinadaiwa kwa wakazi wa Manispaa ya Musoma Mjini, Mkoani Mara ikiwa ni kodi ya Pango la Ardhi.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipofanya ukaguzi wa mfumo wa kodi ya ardhi hivi karibuni Mkoani humo.

Waziri Lukuvi alisema kuwa amekagua mfumo wa kodi wa manispaa ya Musoma mjini ili kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi nchini wanalipa kodi kwa hiari kabla ya hatua za kisheria hazijafuata dhidi yao.

“Nimeagiza kesi za madai ya kodi zitolewe hukumu ndani ya siku moja tu ili wadaiwa waweze kuchukuliwa hatua ya kuuzwa kwa mali zao haraka”, alisema Lukuvi.

Aidha Waziri Lukuvi alimtaka Afisa Ardhi wa Manispaa ya Musoma Bw.Joseph Kamonga kuwasilisha majina ya wadaiwa hao katika Mahakama ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kupiga mnada majengo na mali zao kama wakikaidi kulipa kodi hiyo.

Kwa upande mwingine Lukuvi alifanya uzinduzi wa mpango kabambe (Master Plan) wa Manispaa ya Musoma na kuwapongeza viongozi na watendaji wa Manispaa hiyo kwa kuwa Manispaa ya kwanza nchini kuweza kuzindua mpango huo kutumia kampuni za ndani katika utekelezaji wa mpango huo.

Kufuatia hatua hiyo Waziri Lukuvi amezitaka Manispaa nyingine kutumia kampuni za ndani ya nchi ambazo zimesajiliwa na Wizara ya Ardhi  katika kutekeleza mipango mbalimbali ya ulipaji kodi za ardhi.

Pia Waziri Lukuvi aliiagiza Manispaa ya Musoma kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa mpango kabambe kwa kutumia wataalam wao (wa serikali) au Makampuni ya ndani na kutoa nakala za kutosha ili mpango huo uwafikie wadau wote na kutaka mpango huo utafsiriwe kwa Kiswahili ili Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa waweze kuwafikishia wananchi kwa urahisi.

No comments:

Post a Comment

Pages