HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 21, 2017

WAZIRI MKUU APOKEA TAARIFA YA LOLIONDO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea Taarifa ya Kamati Shirikishi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo ya kushughulikia mgogoro wa matumizi ya ardhi kwenye pori tengefu la Loliondo mkoani Arusha, ambapo atatoa maelekezo baada ya kuisoma.

Amepokea taarifa hiyo leo (Alhamisi, Aprili 20, 2017) katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa Spika, Bungeni mjini Dodoma. Aliiunda Kamati hiyo, Desemba mwaka jana, mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Kiini cha mgogoro huo ni eneo la pori tengefu la Loliondo ambalo linagombewa na wawekezaji, wakulima, wawindaji kwa sababu ni mapitio ya wanyama, chanzo cha maji, mazalia ya wanyama, malisho ya mifugo na makazi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Tate William Ole-Nasha, viongozi wa mkoa wa Arusha, wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.

Wengine ni Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro Bw. Rashid Taka, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa wa Arusha na wilaya ya Ngorongoro, wawakilishi wa wananchi, wawekezaji na asasi za kiraia ambao wote walishiriki katika uandaaji wa taarifa hiyo.

Waziri Mkuu amesema lengo la kamati hiyo ni kutaka kupata muafaka wa matumizi ya rasilimali zilizoko katika eneo hilo ili kila upande uweze kutekeleza majukumu yake bila ya kuathiri mwingine na kuwezesha wananchi wote kunufaika na rasilimali zilizoko katika eneo hilo.

“Serikali inataka watu wote tuwe kitu kimoja katika kutunza maeneo yetu, lakini pia shughuli za wananchi nazo ziweze kuendelea ili Watanzania wote tuweze kunufaika na rasilimali zilizoko kwenye maeneo yetu,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali inapenda kuona maeneo yote nchini yakiwa katika hali ya utulivu  bila ya kuwepo kwa migogoro ya aina yoyote na ikitokea ni vema ikawa inapatiwa ufumbuzi kwa wakati ili shughuli za maendeleo ziweze kufanyika kwa ufasaha.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, APRILI 20, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages