Dande Contanct

TEMBELEA BLOG HII KWA MATUKIO YA KILA SIKU.

CRDB

CRDB
.

Pages

IRINGA DC YATAKIWA KUSIMAMIA SHERIA YA MAZINGIRA

Na Dennis Gondwe, IRINGA
Halmashauri ya wilaya ya Iringa imetakiwa kusimamia sheria ya Mazingira vizuri ili kuondoa uharibifu wa mazingira katika bonde la mto Ruaha mkuu.
Agizo hilo lilitolewa na mwenyekiti wa kikosi kazi namba tatu cha kunusuru ikolojia ya mto Ruaha mkuu ambaye pia ni Katibu Tawala mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu wakati kikosi kazi hicho kilipokutana na timu ya menejimenti ya Halmashauri ya wilaya ya Iringa jana.
Ayubu alisema kuwa Halmashauri ya wilaya ya Iringa inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira. “Ndugu zangu, sheria ya Mazingira lazima isimamiwe ipasavyo. Katika kusimamia vizuri sheria hii wekeni utaratibu mzuri wa kusimamia sheria hii kwa kuziimarisha kamati za mazingira kuanzia ngazi za wilaya, kata na vijiji. Kamati hizi zikiimarishwa utekelezaji wa sheria utakuwa mzuri na wenye kutoa matokeo mazuri zaidi” alisema Ayubu.
Aidha, alizitaka kamati za Mazingira kutekeleza majukumu yake na kutoa taarifa za kazi kwa mamlaka zinazohusika. Alisema kuwa utoaji wa taarifa utaziwezesha mamlaka kuwa na picha kamili ya hali halisi ilivyo na kuwa na uelewa wa pamoja katika kukabiliana na changamoto za kimazingira.
Ayubu aliitaka Halmashauri hiyo kuelekeza miradi yote inayoanzishwa katika Halmashauri hiyo kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji. Alisema kuwa ipo miradi ambayo imekuwa ikianzishwa pasipo kuwaelimisha wananchi juu ya utunzaji wa mazingira na kusababisha uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.
Aidha, aliitaka Halmashauri hiyo kuweka mikakati imara ya kutekeleza uhifadhi wa mazingira. “Halmashauri ya wilaya ya Iringa lazima muweke mikakati madhubuti inayotekeleza katika kusimamia uendelevu wa agenda ya uhifadhi wa mazingira” alisema Ayubu.
Mwenyekiti huyo alimtaka Mwanasheria wa Halmashauri kutoa elimu ya kina ya sheria ya Mazingira na utekelezaji wake kwa kamati ya usalama ya wilaya ili kuiwezesha inapotekeleza majukumu yake katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wa afisa ardhi wa wilaya ya Iringa, Donald Mshani alisema kuwa Halmashauri ya wilaya ya Iringa inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira kutoka na shughuli mbalimbali zikiwemo kilimo ndani ya mita 60 kutoka kingo za mito na uingiaji wa mifugo mingi katika eneo ambalo halina uwezo wa kuihudumia. Alisema kuwa katika kukabiliana na uharibifu huo, halmashauri ya wilaya ya iringa imepanga kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyote vinavyozunguka eneo la bonde la mto Ruaha mkuu ili uhifadhi wa mazingira uweze kutekelezwa kwa mujibu wa sheria na kuwa endelevu.
Awali kaimu mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Abel Mgimwa alizitaja sababu zinazosababisha uharibifu wa mazingira katika Halmashauri hiyo kuwa ni ukataji miti ovyo kwa lengo la kuongeza ukubwa wa mashamba na uchomaji miti kwa ajili ya mkaa. Sababu nyingine alizitaja kuwa ni wafugaji wengi kuingia maeneo ya ukanda wa chini katika Tarafa za Pawaga na Idodi na wananchi kuanzisha mashamba mapya jambo linalosababisha kuondolewa kwa uoto wa asili.
Mgimwa alisema kuwa changamoto hizo suluhisho lake ni mpango wa matumizi bora ya ardhi. Aliongeza kuwa pamoja na mpango huo, sheria ndogo za vijiji kuhusu hifadhi ya mazingira kwa vile vijiji ambavyo havina sheria hizo ili utekelezaji wake uzingatiwe kikamilifu.
Halmashauri ya wilaya ya Iringa ina jumla ya vijiji 133 kati ya vijiji hivyo, vijiji 61 ndivyo vimefanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.

No comments:

Post a Comment