HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 03, 2017

WAZIRI MKUU ATEMBELEA KIWANDA CHA SUKARI TPC

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo Arusha Chini, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro na kukagua baadhi ya miundombinu ya kiwanda pamoja na mashamba.

Akiwa kiwandani hapo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba hivi sasa msimu wa uzalishaji umefungwa na kiwanda kinafanyiwa matengenezo ambapo alishuhudia baadhi ya mitambo ikiwa imefunguliwa na kufanyiwa ukarabati.

Akitoa taarifa juu ya matengenezo hayo mwishoni mwa wiki, Meneja wa Kiwanda hicho, Bw. Pascal Petiot alimweleza Waziri Mkuu kwamba kiwanda hicho kimefungwa kwa zaidi ya wiki sita ili kujiandaa na msimu ujao wa uzalishaji ambao uko karibuni kuanza.

“Hivi sasa ni kipindi cha mvua, tumefunga msimu wa uzalishaji na tunaendelea na ukarabati wa mitambo ili kujiandaa na msimu ujao. Kila mwaka ni lazima tufunge msimu kwa kipindi kifupi, ili kufanya ukarabati kama huu,” alisema.

Akiwa kiwandani hapo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuta mafundi wakifanya matengenezo katika sehemu mbalimbali za kiwanda. Hata hivyo, alionyeshwa mtambo wa kuzalisha umeme wa kiwanda hicho (boiler) ambao unatumia mabaki ya miwa yaliyokwisha kamuliwa juisi (bagasse) ambayo huchomwa na kuchemsha maji ili kupata mvuke unaosukuma jenereta.

“Tunatumia mabaki ya miwa badala ya kuni, joto linalozalishwa linafikia nyuzijoto 450 na kuweza kuzalisha megawati 17.5 wakati kiwanda kikiwa kinafanya kazi. Matumizi yetu kwa ajili ya kiwanda, makazi ya watumishi na vijiji vya jirani yanafikia megawati 12, na tunawauzia TANESCO megawati 4 ambazo wanaziingiza kwenye gridi ya Taifa,” alisema Bw. Jaffari Ali Omari ambaye ni Afisa Utawala Mtendaji.

Bw. Omari alimweleza Waziri Mkuu kwamba umeme unaozalishwa na kiwanda hicho ni mwingi kuliko unaozalishwa na mabwawa ya Hale na Nyumba ya Mungu yakijumuishwa kwa pamoja. “Hale inazalisha megawati nane na Nyumba ya Mungu inazalisha megawati tatu,” alisema.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Bw. Robert Baissac alisema uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda hicho umepanda kwa asilimia zaidi ya 200 tangu wachukue kiwanda hicho mwaka 2000.

Alisema wakati wanaanza, kiwanda kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 36,000 kwa mwaka na wakati wanakinunua walitakiwa kuongeza uzalishaji kwa asilimia 100 kwa kufikisha tani 72,000 za sukari. “Tuliweza kuvuka lengo hilo tangu mwaka 2007 na hivi sasa tumeweza kuzalisha tani 111,800 katika msimu uliopita,” alisema.

“Tunatumia mbegu bora zilizofanyiwa utafiti na majaribio hapa hapa kiwandani. Tunatumia mbolea na njia za umwagiliaji ili kuhakikisha hadhi ya miwa yetu ni ya kuridhisha, na inayoweza kutupatia kiwango kikubwa cha sukari,” alisema.

Akitoa maoni ya jumla, Waziri Mkuu aliwataka wafanyakazi wa kiwanda hicho wafanye kazi kwa bidii na kujituma na kuhakikisha wanaongeza tija katika uzalishaji wao.

“Msisitizo wa Serikali ni kuwasihi Watanzania tubadilike, tuchape kazi ili tuweze kuongeza tija mahali pa kazi,” alisema Waziri Mkuu. 

Alikuwa akijibu hoja ya Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi kiwandani hapo (TASIWU), Bw. Bilal Omar Mchomvu ambaye aliomba Serikali iangalie uwezekano wa kuondoa makato ya kodi kwenye bonasi na overtime wanazolipwa na kiwanda hicho.

Kuhusu haki za wafanyakazi kiwandani hapo, Bw. Mchomvu alimweleza Waziri Mkuu kwamba chama cha wafanyakazi kina mahusiano mazuri na menejimenti ya kiwanda na kwamba kila miezi mitatu wanakutana na wafanyakazi hao kama sheria inavyotaka.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MEI 3, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages