HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 15, 2017

KULIFUNGIA GAZETI LA MAWIO KWA MIEZI ISHIRINI NA NNE (24)

Dar es Salaam, Juni 15, 2017: 

Serikali kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (MB) imelifungia gazeti la MAWIO kutochapishwa kwa miezi Ishirini na Nne (24) kuanzia leo. Mhe. Waziri amechukua hatua hiyo kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari na. 12, 2016.

Hatua hiyo inatokana na gazeti hilo katika toleo na. 196 la 15-21 Juni, 2017 kuchapisha katika ukurasa wa mbele picha za Marais wastaafu Mhe. Benjamin Mkapa na Mhe. Jakaya Kikwete kuwahusisha na sakata la mchanga wa madini.

Aidha, katika ukurasa wa 12 gazeti hilo tena limechapisha makala iliyoandikwa “Lissu: Mkapa, Kikwete Wanaponaje?” kuwatuhumu viongozi hao kuhusika katika sakata la madini wakati ukweli ni kwamba hawakuwa sehemu ya uchunguzi wa Kamati za Rais na wala matokeo ya Kamati hizo hayakuwatuhumu kwa kosa lolote. 

Taarifa ya Mhe. Waziri Mwakyembe kwa Mhariri Mkuu wa gazeti hilo imesisitiza kuwa, licha ya utetezi wao, habari hizo si tu zimekiuka agizo la Serikali, lakini pia zimekiuka vifungu vya 50 (a),(b),(c),(d) na (e) vinavyokataza uandishi wenye dhamira hasi. 

“Sina budi kulifungia Gazeti lako na kukutaka usitishe kulichapisha kwa nakala ngumu au ya mtandaoni kwa kipindi cha muda wa miezi ishirini na nne (24) tangu tarehe ya barua hii kwa mamlaka niliyopewa chini ya Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kifungu 59,” imesema taarifa ya Dkt. Mwakyembe kwenda kwa Mhariri wa MAWIO. 

Natumia fursa hii kuvipongeza vyombo vingi vya habari ambavyo kuanzia leo vimefuata weledi wa taaluma na misingi ya sheria na kutii agizo la Serikali kwa kutowaingiza katika sakata hili pasipo na hoja za msingi viongozi wetu wastaafu.

Imetolewa na:

Dkt. Hassan Abbasi

Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali. 

No comments:

Post a Comment

Pages