HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 16, 2017

TFF YARAHISISHA UPATIKANAJI FOMU ZA UCHAGUZI



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linapenda kuwatangazia wanafamilia wote wa mpira wa miguu wenye nia ya kuwania uongozi kuwa limewarahisishia namna ya kupata fomu baada ya tovuti ya TFFwww.tff.or.tz kuwa kwenye marekebisho.
Kwa wanafamilia ambao wapo nje ya Dar es Salaam, wanaotaka fomu hizo kwa sasa hawana budi kutuma ujumbe wa barua pepe kwenda kwenye anwani ya info@tff.or.tz na moja kwa moja atajibiwa kwa kupata fomu hizo ziliazoanza kutolewa leo Juni 16, mwaka huu. Kwa walioko Dar es Salaam, wanaweza kupata fomu hizo katika ofisi za TFF zilizo Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Mwanafamilia wa mpira wa miguu mwenye nia ya kugombea ataweza kufungua fomu hizo na kuzijaza huku akifuata utaratibu wa kulipia kwenye nambari ya akaunti 01J1019956700 katika Benki ya CRDB.

Zoezi hili kuchukua fomu na kuzirejesha fomu lililoanza leo Juni 16, litafikia kikomo Juni 20, mwaka huu kwa mujibu wa Kanuni ya 10.8 ya Uchaguzi kama ilivyoanishwa kwenye katiba ya TFF.

Mara baada ya kulipia, Mgombea atawajibika kuwasilisha stakabadhi ya malipo kutoka benki na kupewa fomu ya nafasi husika.

Gharama za kuchukulia fomu ni.
1.   Rais TSHS 500,000/=
2.   Makamu wa Rais TSHS 300,000/=
3.   Wajumbe wa kamaki ya utendaji TSHS 200,000/=

RAIS MALINZI AMSHUKURU MGOYI

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Jamal Malinzi amempongeza Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF, Ahmed Mgoyi kwa utumushi mara baada ya kutangaza kutowania nafasi yoyote ya uongozi.

Mjumbe Mgoyi anayewakilisha Mikoa ya Kigoma na Tabora aliandika waraka jana Juni 15, 2017 akielezea kutogombea tena katika Uchaguzi wa TFF unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.

“Nimefanya kazi na Wajumbe wangu wote wa Kamati ya Utendaji. Tumefanya kazi kwa uadilifu mkubwa. Wakati Tukielekea kwenye uchaguzi, mwenzetu ametangaza kutogombea tena, lakini kwa namna nilivyofanya naye kazi, kwangu mimi naamini anahitajika mno, lakini uamuzi wake ni mwisho unakuwa ni wa kwao.

“Naamini kwamba bado ni mwanafamilia wa mpira wa miguu na pindi atakapohitajika kwa lolote lile kama vile ushauri na masuala mengine, basi hatutasita kuwafuata kwa sababu lengo ni kujenga na kuendeleza mpira wetu,” amesema Malinzi.

Katika ujumbe wake, Rais Malinzi amesema kwamba hadhani kama Mgoyi hao atasita au kukataa kutoa ushirikiano kwa uongozi wa shirikisho pindi akihitajika kutoa msaada wao wa mawazo na ushauri.

Rais Malinzi amemtakia kila la kheri katika majukumu yake mengine aliyojipangia kuyafanya huku akiwa bado mwanafamilia wa mpira wa miguu.

PONGEZI KWA FRANCIS AMIN MICHAEL

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi, amempongeza Francis Amin Michael kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Sudan Kusini (SSFA).

Amin - Mfanyabiashara aliyepata kuwa Mjumbe wa Bodi ya timu Atlabara FC, alishinda nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Juba ambako aliwashinda Lual Maluk Lual na Arop Joh Aguer baada ya kuvuna kura 22 kati ya 34.

Amin anamrithi Chabur Goc Alei, ambaye hakutetea nafasi hiyo.

Katika salamu za pongezi, Rais Jamal Malinzi amesema kwamba ana imani na Amin katika nafasi hiyo kwa kuwatumikia vema Wana Sudan Kusini kama alivyoahidi mara baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

Rais Malinzi anaamini kwamba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile Serikali ya Sudan Kusini, ataendeleza mpira wa miguu hususani katika Baraza la Mpira wa Miguu la Afrika Mashariki ambako Tanzania na Sudan Kusini ni nchi wanachama.


MCHAKATO WA UCHAGUZI WA CHAMA CHA SOKA LA WANAWAKE TANZANIA (TWFA)

Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Wanawake (TWFA), leo Juni 16, 2017 imetangaza rasmi Uchaguzi wa chama hicho utakaofanyika Julai 8, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, George Mushumba amesema kwamba fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hizo zitaanza kutolewa Juni 19, mwaka huu na kwamba mwisho wa kuchukua na kurudisha ni Juni 22, mwaka huu saa 10.00 jioni. Ratiba kamili kuelekea uchaguzi huo ni kama ifuatavyo:-

Juni 23, 2017- Kamati ya Uchaguzi kupitia majina ya wagombea walioomba kugombea nafasi mbalimbali.

Juni 24, 2017- Kamati ya Uchaguzi kutangaza majina ya wagombea waliostahili au waliotimiza taratibu za uchaguzi kwa mujibu wa katiba
                       au kanuni za TWFA.

Juni 26 na 27, 2017- Kupokea pingamizi kati ya saa 4:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.

Juni 28, 2017- Kamati ya Uchaguzi kupitia pingamizi kama zimewasilishwa.

Juni 29, 2017-  Kamati kutoa majumuisho ya pingamizi kama ziliwasilishwa na wadau.

Juni 30, 2017-  Usaili kwa wagombea waliotangazwa

Julai 01, 2017- Kutangaza majina ya wagombea waliopitishwa

Julai 02, 2017-Kamati kupokea rufaa

Julai 03, 2017-  Kamati kupitia rufaa kama zimewasilishwa

Julai 04, 2017   Kamati kutangaza orodha ya mwisho ya wagombea

Julai 04 hadi 07, 2017-Wagombea kufanya kampeni kwa kuzingatia maadili

Julai 08, 2017- Uchaguzi Mkuu wa TWFA

Mushumba amesema kwamba nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji. Sifa ya elimu kwa wagombea wote ni kidato cha nne.

Kwa nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Katibu Msaidizi fomu zitanunuliwa kwa Sh 200,000 wakati nafasi za Mweka Hazina, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji fomu zitapoatikana kwa Sh 100,000. Fomu zitapatikana ofisi za Hosteli ya TFF zilizoko Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

.……………………………………………………………………………………………..
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Pages