HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 25, 2017

Wataka adhabu ya ubakaji iwe kifungo cha Maisha

Na Talib Ussi ,Zanzibar 

WAJUMBE wa kamati mbili za baraza la Wawakilishi wamesema kuwa imefika wakati hivi sasa adhabu ya kesi za ubakaji iwe ni kifungo cha maisha au adhabu ya kifo kwa wahusika wa matendo hayo.

Wajumbe hao ambao ni kutoka kamati ya Ustawi wa jamii na ile ya Wanawake na watoto walidai hivyo kwa adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa kesi hizo imepitwa na wakati na hivi sasa ipo haja ya kubadilishwa.

Walitoa kauli hiyo Visiwani hapa wakati walipofanya mazungumzo ya pamoja kati ya wajumbe hao na asasi za kiraia za kutetea haki za wanawake na watoto juzi ikiwa ni muendelezo wa kuadhimisha motto wa Afrika.

Walieleza kuwa kutokana kudumu kwa muda mrefu adhabu inaonekana vitendo vya ubakaji vimekuwa vikishamiri siku hadi siku Visiwani Zanzibar.

“Adhabu ya kifungo cha miaka 30 hakiendani kabisa na athari ya tendo la ubakaji kwa muhanga kwani Mtoto anaefanyiwa kitendo hicho huathirika kisaikolojia,kiakili na kimwili” alisema Mwenyekiti wa kamati ya Wanawake na Watoto Ali Suleiman Shihata.

Alieleza kuwa licha ya kuwekwa kwa adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 30 lakini Mahakama za Zanzibar zimekuwa hazitowi adhabu hiyo na kesi nyingi za ubakaji zimekuwa zikitolewa hukumu ndogo ya chini ya miaka saba au mtuhumiwa kuachiwa huru.

“wasi wasi wangu kesi hizi zimeingiliwa Rushwa iliyokithiriri ndio maana kesi zimekuwa zikitupwa au watuhumiwa kuhukumiwa adhabu ndogo” alieleza Shihata.

alifahamisha kuwa uwezo wa kifedha unaathiri sana katika kesi hizi za ubakaji kwa sababu rushwa imetawala kila mahala, lakini pia jamii bado imekuwa na ugumu kutoa ushahidi mahakamani.

Mwenyikiti wa kamati ya Ustawi wa jamii Dk Mwinyihaji Makame, alisema kuwa jambo linalokera ni kesi za udhalilishaji kuchukuwa muda mrefu Mahamakani hali hiyo imekuwa ikiwavunja moyo wanajamii hasa wahanga wa kese hizo.

“Masikini ya Mungu anahangaika anakwenda Mahakamani na kurudi anaambiwa kuwa jaji au hakimu anaesikiliza kesi amesafiri au hayupo na kumfanya mlalamikaji kuaza kukata tama” alisema Dk Mwinyihaji ambae pia ni Mwakilishi wa jimbo la Dimani

Alisema majaji na mahakimu wanaoendesha kesi mahakamani wanalipwa mishahara kila mwisho wa mwezi lakini wananchi wanaokwenda kutoa ushahidi au kufuatilia mwenendo wa kesi hawana malipo ya fedha na ndio maana watu wanaona bora waendelee na shughuli zao za kujitafutia kipato kuliko kwenda na kurudi mahakamani bila ya manufaa.

Aidha alipongeza hatua ya serikali ya kuwanyima dhamana watuhumiwa wa vitendo vya udhalilishaji wa watoto na hiyo ni hatua nzuri kwa sababu kitendo cha kupewa dhamana kimekuwa kikiwapa majigambo watuhumiwa wa kesi hizo.

Nae mjumbe wa kamati hiyo ambae pia ni mwakilishi wa Viti maalum,Zainab Abdallah alilitupia lawama jeshi la polisi kuwa bado baadhi ya askari wake hawazingatii maadili yao ya kazi kwa kesi za udhalilishaji wa watoto hasa watoto wenye ulemavu wa akili.

“Utamkuta mtoto mwenye ulemavu wa akili amefanyiwa udhalilishaji Polisi anaipokea kesi na kumtazama kwa dharau kutokana na ulemavu wake”alisema Zainab.

Alisema watu wenye ulemavu wa akili hata kama watakuwa na umri wa miaka 18 au zaidi lakini akili zao zinaingia na kutoka kwa hivyo mambo yao wanayoyafanya yanakuwa ni ya kitoto hivyo wanahitaji msaada.

Akiwasilisha mapendekezo hayo kwa niaba ya asasi hizo Dk Mzuri Issa Mkurugenzi wa Tamwa kwa upande wa Zanzibar,alisema ni vyema wajumbe wa baraza la wawakilishi,wanaharakati na mashirika ya kijamii kukutana kabla ya kuwasilishwa marekebisho ya sheria hasa yanayohusu masuala ya watoto na jinsia.

Asasi za kiraia ambazo zinatetea haki za wanawake na watoto ambao ndio waandaaji wa mkutano huo, walipendekeza kuwa sheria zifanyiwe marekebisho hasa sheria ya mwenendo wa kesi za jinai ili iwe kisheria kesi za ukatili dhidi ya watoto kuwa ni miongoni mwa kesi ambazo hazina dhamana.

No comments:

Post a Comment

Pages