HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 09, 2017

Watanzania Tumuunge Mkono Rais Magufuli Kuikataa Mikataba Mibovu – Kamara

Na. Lilian Lundo - MAELEZO

Watanzania wameombwa kushikamana kumuunga mkono Rais Dkt. John Pombe Magufuli juu ya hatua anazochukua dhidi ya wanaofaidika na mali za Watanzania kutokana na mikataba mibovu.

Wito  huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mwinjilisti Kamara Kusupa  alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu watu wanaopinga hatua alizozichukua Rais Magufuli za kuzuia makontena 277 yenye ‘makinikia’ kusafirishwa nje ya nchi. 

Mwinjilisti Kamara amesema kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kumuunga mkono Mheshimiwa Rais ili watu wanaompinga wajue hawashindani na Rais peke yake wala Serikali bali wanashindana na Watanzania wote.

“Watanzania tuungane kuikataa mikataba inayolazimisha nchi yetu iendelee kudhulumiwa na kukandamizwa, tuupinge ukoloni uliorudishwa kwa mlango wa nyuma kupitia ndugu zetu wachache wa awamu zilizopita waliokosa umakini na uaminifu,” amefafanua Mwinjilisti Kamara.

Aliendelea kwa kusema, Watanzania wamechoka na uwekezaji usionufaisha nchi badala yake kuwanufaisha wawekezaji na kuwapa kiburi cha kuwanyanyasa Watanzania hadi kufikia hatua ya kupinga waziwazi tena hadharani hatua halali zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya mikataba hiyo mibovu.

Mwinjilisti huyo amesema, Mkurugenzi wa ACACIA amemkosea Rais Magufuli kwa kutaka iundwe tume huru ifanye  upya uchunguzi wa makinikia wakati Rais alishaunda tume ya wataalamu na kujiridhisha na thamani ya makinikia hayo yaliyokuwa yakisafirishwa nje ya nchi.

Aidha amesema, jeuri aliyoonyesha mwekezaji huyo na baadhi ya wawekezaji inaonyesha wanawanyanyasa Watanzania waishio kwenye maeneo waliyowekeza kutokana na wawekezaji hao kupewa uhuru unaozidi kawaida na haki ya ziada iliyowafanya wasahau kwamba Tanzania ni mali ya Watanzania.

Mwinjilisti Kamara amemuomba Rais Magufuli kuunda tume huru itakayopitia upya mikataba yote inayogusa rasilimali za nchi kutokana na mikataba hiyo kuonekana kuiondolea nchi uhuru wake pamoja na kutotambua kama Tanzania ni dola huru yenye haki na mali zake.

Vile vile amewataka wananchi kushikamana kwa nguvu moja kuikataa mikataba iliyosainiwa na wapenda rushwa, kwa kuwa ndio waliosababishia umaskini na kuipunguzia Serikali uwezo wa kuhudumia wananchi wake.

No comments:

Post a Comment

Pages