HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 15, 2017

WAZIRI MKUU ATAKA MAAFISA MIFUGO WABADILIKE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka maaafisa mifugo wote wa wilaya na mikoa wabadilike ili sekta hiyo iweze kuongeza mchango wake kwenye pato la Taifa.

“Katika ziara zangu za mikoani nimekuwa nikionesha kutoridhishwa kwangu na utendaji kazi wenu, na hasa jinsi tunavyoendesha ufugaji hapa nchini. Mmeacha kazi ya kuwaongoza wafugaji, wanafanya wanavyotaka. Tunahitaji kuona mabadiliko makubwa katika sekta hii,” amesema. 

Ametoa agizo hilo leo mchana (Alhamisi, Juni 15, 2017) wakati akizungumza na maafisa mifugo kutoka wilaya zote na mikoa yote wanaohudhuria kikao alichokiitisha ili wajadili namna wanavyoweza kubadili uchungaji na kufanya uwe ufugaji. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Waziri Mkuu amesema takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha Tanzania ni nchi ya tatu barani Afrika na ya 11 duniani kwa ufugaji, ikiwa na ng’ombe takriban milioni 24, nyuma ya Ethiopia yenye ng’ombe milioni 54 na Sudan yenye ng’ombe 41.

“Wakati sekta ya mifugo inatoa mchango usiozidi asilimia 10 kwenye Pato la Taifa, wenzetu Ethiopia sekta hiyo hiyo inachangia asilimia 14 kwenye pato lake na asilimia 16 ya fedha za kigeni. Nchi kama Botswana na Namibia, nazo zinafanya vizuri kwenye sekta ya mifugo, pamoja na kwamba wana mifugo michache, na eneo dogo la ardhi,” amesema.

“Ni lazima tuanze kufikiri tofauti na kujitathmini kama kweli tunawatendea haki Watanzania waliogharamia elimu yetu na wanaoendelea kutulipa mishahara. Ningependa kupata ufahamu wenu wa kitaalam mna mipango gani kuinua sekta hii kwa kuwafanya wafugaji wa Kitanzania wawe wafugaji wanaotumia utaalam na hatimaye wao wenyewe na Taifa zima linufaike kwa kupunguza umaskini,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amewataka maafisa hao wabadili mitazamo yao na waache kufanya kazi kwa mazoea. “Ni lazima mtafute ufumbuzi wa kudumu kuhusu utatuzi wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji; na wafugaji na wahifadhi wa mapori tengefu au mapori ya akiba.”

Amewataka wajipange kuongeza uzalishaji wa mitamba na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuendelea kuzalisha mitamba ili kuhamasisha ufugaji wa kisasa. Na pia watenge, wapime na kuwamilikisha wafugaji maeneo ya ufugaji.

Amesema ili kukuza sekta hiyo hawana budi kutoa elimu ya matumizi ya teknoljia ya uhamilishaji, kuendeleza na kukuza masoko ya mifugo na mazao yake kwa kujenga viwanda. “Afisa mifugo ni lazima ujue kwenye Halmashauri yako kuna minada mingapi na inafanyika wapi.  Kwenye bajeti hii, tumeondoa kodi ya makanyagio, naamini hii itaongeza chachu ya wafugaji kupelekea mifugo yao minadani,” amesema. 

Amewataka pia waendelee kuimarisha huduma za ugani katika ngazi za kata na vijiji na kuhakikiasha wanaanzisha mashamba darasa ya mifugo. “Jipangeni kuanzisha mashamba darasa ya malisho katika kila Halmashauri. Kila eneo mnaweza kuwa na shamba darasa kwa kuchagua mfugaji mmoja au wawili ili wawe ndiyo mashamba darasa kwa wenzao,” amesema.

Mkutano huo ambao umehudhuriwa na maafisa mifugo wa wilaya 185 na Maafisa Tawala Wasaidizi wa Mikoa (wanaoshughulikia masuala la mifugo) zaidi ya 20, umehudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, na Naibu Waziri wake, Bw. Willian Tate Ole Nasha, Makatibu Wakuu wa Wizara za Kilimo na TAMISEMI, Wakuu wa Mapori ya Akiba, Wakurugenzi wa Wizara ya Viwanda na Biashara na taasisi zinashughulika na maliasili; na wakuu wa vyuo vya wanyamapori.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuhutubia maafisa hao, Waziri wa Nchi (OR – TAMISEMI), Bw. George Simbachawene alisema migogoro na chuki vinatokea kwa sababu wahusika hawajaoa​

Tuchukue mfano, mtu akiwa na ng’ombe 1,000 katika eneo fulani. Kama uzalishaji wake ukioanishwa na uchumi wa eneo husika, mafanikio lazima yatakuwa ni ya eneo lile na siyo ya mtu binafsi,” alisema.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.            
ALHAMISI, JUNI 15, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages