HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 20, 2017

GGM yanufaisha wazawa sekta ya madini

Programu ya utoaji ajira kwa wahitimu mbalimbali wa vyuo vikuu inayoendelea kwa kasi chini ya uratibu wa Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM) kwenye nyanja za uchakataji madini, ufundi umeme, ufundi wa mitambo mizito ya uchimbaji, ufundi mitambo, na elimu ya miamba kwa awamu ya pili umeanza kwa mafanikio makubwa.

Programu hiyo ambayo imetengewa na GGM zaidi ya shilingi milioni 340, kwa sasa imeingia kwenye awamu ya pili lengo likiwa ni kuajiri wahitimu wa vyuo vikuu wenye vipaji nchini na kuwapa mafunzo ya haraka ili kukuza ujuzi wao kwa muda wa miaka miwili.

Akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa GGM, Tenga Tenga, alisema programu hiyo inakusudia kuwapa vijana wa Kitanzania fursa ya kuendeleza vipaji vyao kwenye sekta ya madini kwa kuwapatia nafasi ya kujifunza ujuzi mpana kitaaluma ili kujiendeleza wao wenyewe na kufikia malengo yao.

“Mgodi wa Dhahabu wa Geita unaamini kwamba kujenga uwezo kwa watumishi wetu pamoja na kuajiri wahitimu wa vyuo vikuu wenye vipaji ni jambo muhimu lenye kuleta tija na kusaidia mkakati wetu wa kuendeleza rasilimali watu na maendeleo ya jamii inayotuzunguka,” alisema Tenga

Aidha, akifafanua zaidi kuhusu programu hiyo alisema kwa sasa ipo kwenye awamu ya pili baada ya kufanikiwa kubakiza asilimia 70 ya wahitimu katika awamu ya kwanza.

Hata hivyo hadi sasa kuna wahitimu wapya 12 viwandani wanaoendelea na mafunzo, na tayari wahitimu hao wapya wameshamaliza baadhi ya mafunzo ikiwemo mafunzo kazini, mafunzo mchanganyiko, na uzoefu kwenye migodi.

Mwezi Julai mwaka 2009, Mgodi wa GGM uliwasiliana na vyuo vikuu kadhaa vya Tanzania, vikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) pamoja na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) katika kufanikisha programu hiyo.

Alisema wahitimu kadhaa walituma maombi na kufanyiwa usaili ili kujiunga kwa nia ya kujiendeleza na kupata mafunzo kazini, waliofanya vizuri walipewa ajira ya muda wa miaka miwili kabla ya kupewa ajira ya kudumu kutokana na tathmini ya utendaji wao iliyofanywa na GGM.

“Wahitimu wanaochaguliwa hupewa mafunzo ya haraka na kupangwa kwa mzunguko kwenye vitengo mbalimbali vya uchimbaji madini ili kuwapa mafunzo na uelewa wa mambo mbalimbali ya utendaji mahususi kwenye kampuni. Baada ya miaka miwili, wahitimu wanaofanya vizuri hufikiriwa kupewa nafasi za juu kwenye fani zao na baadaye hupatiwa fursa za kupata uzoefu wa kimataifa kwenye kampuni ya AngloGold Ashanti,” alisema Tenga

No comments:

Post a Comment

Pages