HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 22, 2017

MKE WA WAZIRI MKUU APONGEZA WANAWAKE WAJASIRIAMALI ILEJE

MKE wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewapongeza wanawake wa wilaya ya Ileje mkoani Songwe kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali.

Ametoa pongezi hizo leo (Jumamosi, Julai 22, 2017) wakati akiwasalimia wananchi wa wilaya ya Ileje katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Stendi.

Ametoa pongezi hizo baada ya kushiriki katika ukaguzi wa vikundi mbalimbali vya wanawake wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali wilayani Ileje.

Mke wa Waziri Mkuu ambaye ameambatana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ziara ya kikazi mkoani Songwe, amesema ujasiriamali ni mkombozi kwa wanawake.

Mama Mary amesema amefarijika kuona wanawake wengi wakishiriki katika shughuli za ujasiriamali kwa kuwa zinalenga kuwaongezea kipato na kuwakwamua kiuchumi.

Mmoja wa wajasiriamali hao, Bi. Riziki Sunday amesema shughuli hizo za ujasiriamali zimemuwezesha kumudu mahitaji ya familia yake, hivyo kuondokana na utegemezi.

Bi. Riziki amesema kuwa miongoni mwa faida alizozipata kutokana na ujasiriamali ni pamoja na kujenga nyumba, kusomesha watoto na kuongeza mashamba.

Pia Bi. Riziki ametumia fursa hiyo kuwashauri wanawake wenzake kujiunga na vikundi vya ujasiriamali ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JULAI 22, 2017

No comments:

Post a Comment

Pages