HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 18, 2017

TAIFA STARS YAIFUATA RWANDA

Kikosi cha timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kinatarajiwa kwenda Kigali, Rwanda kesho Jumatano mchana kikitokea Mwanza, Tanzania.


Taifa Stars iliyokuwa jijini Mwanza kwa kambi kabla ya kucheza mchezo wa kwanza dhidi ya Rwanda Jumamosi iliyopita, itapitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere kwenda Rwanda.

Stars itaondoka Mwanza kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania majira ya saa nne asubuhi na kuwasili Dar es Salaam majira ya saa sita mchana kabla ya kuunganisha ndege ya Rwanda majira ya saa nane alasiri kwenda Kigali, Rwanda.

Inakwenda Kigali kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Rwanda maarufu kama Amavubi kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN 2018). Fainali za CHAN mwakani zitafanyika nchini Kenya.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. Mshindi wa jumla katika michezo miwili, atakuwa amesonga mbele hivyo kukutana na Uganda mwezi ujao.

Katika mchezo huo wa marudiano utakachezwa Kigali Rwanda, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga atamkosa beki wake wa kulia, Shomari Kapombe anayesumbuliwa na mguu alioumia katika mchezo kwanza.

TAARIFA YA KAMATI YA UCHAGUZI TASMA

Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Wataalamu wa Tiba za Michezo (TASMA), kimetangaza majina ya waliochukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Agosti 5, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya chama hicho, Leslie Liunda wanaowania uenyekiti ni Joakim Mshanga, Usubene Kisongo na Biyondo Mgome ilihali kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti, amejitokeza Magreth Mtaki pekee.

Wale wanaotaka ukatibu mkuu wa chama hicho ni Suphian Juma na Nassoro Matuzya waliojitokeza huku nafasi ya ukatibu msaidizi inawaniwa na Alfred Mchinamnamba.

Nafasi Mweka Hazina inawaniwa Alex Gongwa huku Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF inawaniwa Richard Yomba na Cosmas Kapinga ilihali Ujumbe wa Kamati ya Utendaji wamo Paschal Itonge na Mwanandi Mwankemwa.

Kwa mujibu wa ratiba ya mchakato wa uchaguzi huo kuanza leo na kesho (Julai 18, 2017 na Julai 19, mwaka huu) watapokea pingamizi katika ofisi za Omlipiki Maalumu (Special Olympic) zilizopo jirani na Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Kipindi cha usaili kimepangwa kuanza Julai 20, 2017 hivyo wagombea wote wanatakiwa kufika mbele ya kamati ili kusailiwa.


“Mgombea ambaye atashindwa kuhudhuria atakuwa amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi utafanyika Agosti 5, mwaka huu katika Ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam,” amesema Liunda.
……………………………………………………………..………………………….

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Pages