HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 30, 2017

TANZANIA SIYO LANGO LA KUPITISHIA DAWA ZA KULEVYA-MAJALIWA

*Aagiza kuimarishwa kwa ukaguzi wa watu, magari na mizigo mipakani

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya kwenda nchi za nje hivyo ameagiza ulinzi uimarishwe katika mipaka yote.

Amesema kunatabia ya baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kutumia Tanzania kama njia ya kupitisha dawa za kulevya kwa ajili ya kupeleka nchi za  Afrika ya Kusini, Malawi na Zambia.

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Julai 29, 2017) alipozungumza na watumishi wa kituo cha forodha cha Kasumulu kilicho katika mpaka wa Tanzania na Malawi wilayani Kyela.

Waziri Mkuu alisema ili kuhakikisha jambo hilo linadhibitiwa ni vema ukaguzi wa watu wanaopita kwenye maeneo hayo pamoja na mizigo ukaimarishwa.

“Endeleeni kufanya upekuzi wa kina wa magari, watu na mizigo yote yote katika mipaka yetu. Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya na Serikali haitakubaliana na jambo hilo.”

Pia aliwataka viongozi hao kuhakikisha biashara zote za magendo zinazifanyika mipakani, zikiwemo za kubadilisha fedha zinadhibitiwa kwa kuwa zinaikosesha Serikali mapato.

Alisema ni vema yakawepo maduka ya kubadilishia fedha katika maeneo hayo ili kudhibiti biashara hiyo ambayo kwa sasa inafanywa kimagendo huku Serikali ikikosa kodi.

“Biashara za magendo zidhibitiwe katika maeneo haya na yaanzishwe maduka ya kubadilishia fedha ili biashara hiyo ifanyike kihalali. Pia imarisheni vyanzo vya mapato.”

Pia Waziri Mkuu aliwataka Maofisa wa Uhamiaji katika mikoa hiyo ya mipakani kuhakikisha wanadhibiti uingiaji holela wa raia wa kigeni kwa lengo la kuimarisha ulinzi nchini.

Waziri Mkuu alisema katika baadhi ya maeneo kwa sasa zimeanza kuonekana silaha ambazo hapo awali hazikuwepo na ndizo zinazosadikiwa kutumika katika matukio ya kihalifu.

Awali, Bw. Taniel Magwaza ambaye ni Afisa Mfawidhi wa Uhamiaji alisema watahakikisha wanafanya kazi kwa weledi katika kupambana na biashara za magendo kwenye mpaka huo.

Alisema mbali na kupambana na biashara za magendo pia watadhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu kwa kushirikiana na watumishi idara zote waliopo katika mpaka huo wa Kasumulu.

Bw. Magwaza alisema katika doria zilizofanywa mwaka 2016/2017 jumla ya wahamiaji haramu 87 walikamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Alisema wahamiaji hao walitokea nchi za Malawi (30), Ethiopia (47), Burundi (6) Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) (4), ambapo baadhi walirudishwa makwao na wengine walifungwa katika Gereza la mkoa wa Mbeya.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 30, 2017
                              
       

No comments:

Post a Comment

Pages