Dande Contact

TEMBELEA BLOG HII KWA MATUKIO YA KILA SIKU-MOBILE +255 713 623 958 / +255 784 623 958 EMAIL dande15us@gmail.com

Halotel


CRDB

CRDB
.

Pages

UFAFANUZI KUHUSU PROPAGANDA NA UPOTOSHAJI WA TUNDU LISSU

Dodoma, Julai 18, 2017
 
Vyombo mbalimbali vya habari leo vimemnukuu Mbunge wa Singida Mashariki Ndugu Tundu Lissu ambapo pamoja na mambo mengine, huku wakati fulani akitumia lugha za kuudhi, uchochezi na kejeli, ameituhumu Serikali kuwa inabana demokrasia nchini.
 
Tunachukua fursa hii kumshauri Ndugu Tundu Lissu ambaye pia kwa nafasi yake kama Wakili wa Mahakama Kuu ni Afisa wa Mahakama walau basi atekeleze wajibu wake wa kusimamia weledi badala ya kila wakati kuyatazama mambo kwa jicho la siasa.
 
Madai kwamba Serikali inakandamiza demokrasia ni propaganda tu za kisiasa. Hii ni kwa sababu Ndugu Lissu anaonekana kuchanganya kati ya haki katika demokrasia ambazo hata yeye amezitumia kuongea na wanahabari bila tashtiti kwa upande mmoja na misingi ya wajibu kwa upande mwingine ambayo kila mmoja, iwe Tanzania au kwingineko duniani, anayo na pale anapoikiuka hatua huchukuliwa.
 
Tofauti na upotoshaji wa Ndugu Lissu, Tanzania ikiwa nchi kiongozi Afrika na duniani katika kuenzi demokrasia na kupigania haki, si tu inaendelea kuenzi misingi hiyo bali pia imechukua hatua za wazi kuhakikisha kuwa misingi hiyo inalindwa na pale mtu na hata taasisi zinapokiuka basi mkondo wa sheria, jambo muhimu katika utawala bora,  huchukua nafasi yake.
 
Mintaarafu tu, ikiwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), Tanzania imeridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 na huwasilisha taarifa zake za utekelezaji wa demokrasia na haki za binadamu katika Kamisheni ya UN ya Haki za Binadamu.
 
Kikanda, Tanzania ikiwa mwanachama kiongozi wa Umoja wa Afrika (AU) imeridhia pia Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na ni miongoni mwa nchi za kwanza kabisa Afrika kukubali kushtakiwa na wananchi wake kwa kuridhia itifaki ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na pia kukubali kufanyiwa ukaguzi katika utawala bora kupitia Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
 
Kitaifa, pamoja na kuruhusu tasisi anuai za umma na binafsi, Serikali ya Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache Afrika yaliyotunga sheria ya ndani ya nchi inayowapa wananchi wake haki ya kuishitaki Serikali au watu wengine wanapoona wamevunjiwa haki zao za kidemokrasia au kibinadamu (The Basic Rights and Duties Enforcement Act, 1994).
 
Katika mawanda ya mikataba ya kimataifa, tofauti na upotoshaji wa Ndugu Lissu, misingi yote ya uhuru iwe demokrasia, kujieleza na haki nyingine za kibinadamu imewekewa katika mtindo wa haki na wajibu na mataifa yote, ikiwemo Tanzania na yale anayodhani yatamsaidia, huchukua hatua madhubuti kulinda haki hizo lakini pale wajibu unapokiukwa hatua kali huchukuliwa.
 
Ndio maana tumejiuliza hivi anapotoa mfano wa Bunge kutokuwa “live” (mbashara) siku nzima kuwa ni dalili ya demokrasia kubanwa nchini Ndugu Lissu amejiuliza hayo mataifa anayojaribu kushawishi yaisuse Tanzania ni mangapi katika nchi zao ambako Bunge huoneshwa mbashara walau kwa takribani saa mbili au zaidi kwa siku kama Tanzania inavyofanya sasa?
 
Tumeona pia akikejeli mahakama za nchi. Hivi Ndugu Lissu amejiuliza ni mara ngapi yeye binafsi au wabunge wenzake wa upinzani wameshinda kesi katika mahakama anazozituhumu kila siku kuwa haziko huru?
 
Ni kwa sababu hizi basi tunamuasa Ndugu Lissu na wananchi kwa ujumla kujiepusha na propaganda, kejeli na uzushi usio na msingi dhidi ya Serikali au taasisi zake na pale ambapo wanadhani kuna haki zimekiukwa badala ya kuvunja sheria ni vyema kutafuta haki kupitia mkondo wa kisheria ambao tumeuainisha hapo juu.
 
Serikali itaendelea kuenzi na kuilinda misingi ya demokrasia, uhuru wa watu na kuwapa fursa wananchi kushiriki katika uchumi wa nchi hasa wakati huu wa mageuzi makubwa ya kiutendaji chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli lakini haitavumilia mtu yeyote au kikundi chochote kitakachojaribu kutumia uhuru wowote vibaya ili tu kukwaza azma hiyo ya Taifa.
 
Imetolewa na:
signature2
 
 Dkt. Hassan Abbasi
 
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali. 

No comments:

Post a Comment