HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 14, 2017

WAZIRI MBARAWA AFANYA ZIARA UWANJA WA NDEGE WA JNIA


NA IRENE MARK

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ameahidi kuufumua uongozi wa Uwanja cha Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa madai ya kukosa uzalendo na ubunifu. 
Pamoja na ahadi hiyo, waziri huyo aliahidi kufumua mikataba minne mikubwa iliyoingiwa kati ya uongozi wa uwanja huo na watoa huduma wengine wanaofanya shughuli zao uwanjani hapo.

Profesa Mbarawa alisema hayo Dar es Salaam muda mfupi baada ya kutembelea vitengo mbalimbali vya uwanja huo kujionea utendaji kazi wao.

Waziri huyo alitembelea JNIA baada ya kupokea malalamiko ya wageni wanaoingia nchini kupitia uwanja huo kutumia muda mwingi kupekuliwa na kumaliza taratibu za kisheria ikiwemo kupata viza.

“Uongozi wa uwanja huu hauridhishi tunataka viongozi wazakendo wenye ubunifu… ipo haja ya kubadili uongozi huu, haiwezekani hata kama una matatizo ndio unakosa ubunifu?

“Hapa ipo mikataba ya hovyo, haijaangalia maslahi mapana ya nchi tunachofanya ni biashara yaani serikali inapata sehemu yake na mfanyabiashara anapata. Mingi ya mikataba haipo vizuri.

“Yaani mtu anafanyabiashara halipi kodi, mwingine analipishwa kodi ya kwa mwezi na analipa anavyotaka, mbona mimi kwenye nyumba ninayokaa nalipa kodi ya mwaka…? ‘Next week’ nitaleta vijana wengine hapa. 

“Mikataba pia ni tatizo tumeweza kubadili Ticts hapa hatushindwi tena ipo minne mikubwa tutawaita walioingia nao mikataba hii, tutajadiliana nao na kupata namna sahihi ya kuendelea nayo huku serikaliu ikipata inachostahili.

“Mkurugenzi wa uwanja ametuambia wanamuhudumia mgeni chini ya dakika moja, sio kweli wageni wanasema wanachelewa sana kwenye ukaguzi,” alisema Profesa Mbarawa.

Alisema JNIA ni kioo cha wageni wanaoingia nchini kujifunza mambo yetu hivyo lazima wajifunze mambo mazuri huku akikubali kuwepo kwa changamoto za udogo wa uwanja kulingana na wageni wanaoingia nchini.

Kwa mujibu wa waziri huyo, malalamiko ya wageni yanawapa chachu ya kufuatilia chanzo cha uzembe na kuhakikisha changamoto za kimfumo wa uwanja zinapungua.

Alisema amebaini kuwepo kwa upungufu wa wafanyakazi wa Benki ya NMNB uwanjani hapo huku akiipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kuongeza watumishi na kuharakisha huduma.
Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Joseph Nyahende alikataa kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwepo uwanjani hapo walitaka kujua changamoto za uongozi wake uwanjani hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya Profesa Mbarawa kuondoka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Salim Msangi alisema ongezeko la wageni linasababisha udhaifu wa huduma.

“Changamoto ya kiwanja hiki ni kuongezeka kwa wageni, ulivyojengwa ulikuwa kwa ajili ya kuhuudumia wageni milioni 1.5 kwa mwaka lakini sasa unahudumia wageni milioni 2.5 kwa mwaka mmoja.

“…Wakati uwanja unajengwa hapakuwa na maduka ndio maana eneo la kuhudumia abiria limekuwa dogo kwa sababu idadi ya wageni nayo imeongezeka.

“Ni kama alivyosema waziri pale kwamba changamoto zipo haziwezi kuisha leo lakini lazima ubunifu uwepo, matatizo madogo madogo yaliyopo ndani ya uwezo wa uongozi yatatuliwe,” alisema Msangi.  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa pili kushoto), akiwa katika ziara ya kutembelea vitengo mbalimbali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Joseph Nyahende na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Salim Msangi. (Picha na Francis Dande).   
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akifafanua jambo wakati wa ziara yake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. 

 Ofisa wa Uhamiaji, Fulgence Mutabasha, akitoa maelezo kwa  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akipata maelezo kutoka kwa Ofisa wa Benki ya NMB katika kaunta ya kulipia Visa.
Waziri Mbarawa akiwa katika ziara yake.
  Ofisa Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Hezbon Gibbe, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alipofanya ziara katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Waziri Mbarawa akimsikiliza mmoja wa wafanyakazi  katika Uwanja wa Ndege wa JNIA. 
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akifafanua jambo. 
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akionyesha kitu wakati ya ziara yake.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara yake.

No comments:

Post a Comment

Pages