HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 22, 2017

WAZIRI MKUU ATOA MIEZI MITATU WALIOJENGA NDANI YA MPAKA WA TANZANIA NA ZAMBIA KUBOMOA NYUMBA ZAO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa wananchi wote waliojenga ndani ya eneo la mpaka wa Tanzania na Zambia kubomoa nyumba zao .
Pia ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuanza kuweka alama za X katika nyumba 252 zilizojengwa ndani ya mpaka huo ili wahusika wazibomoe.

Agizo hilo amelitoa leo jioni (Ijumaa, Julai 21, 2017) alipotembelea eneo la ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha (OSBP) katika mpaka wa Tanzania na Zambia, ambacho kinajengwa na Serikali ya Tanzania na kitagharimu sh. bilioni 12.

“Kuna watu wamejenga ndani ya mpaka wa Tanzania na Zambia na kuendesha biashara zao jambo ambalo ni kinyume cha sheria na linazikosesha Serikali mapato.”

Kufuatia hatua hiyo Waziri Mkuu ametoa muda wa miezi mitatu kwa watu wote waliojenga kuanzia umbali wa mita 50 kutoka Tanzania na mita 50 kutoka Zambia kuzibomoa nyumba hizo kwa hiari.

“Hatuna msamaha kwa watu waliojenga katika eneo hili kwa sababu wamesababisha tupoteze kodi nyingi, hivyo baada ya kumalizika muda huo mamlaka husika zibomoe nyumba zote zitakazosalia.”

Awali Waziri Mkuu alikutana na Mkuu wa wilaya ya Nakonde nchini Zambia, Bw. Field Simwinga ambaye alisema wamekubaliana na utekelezaji wa agizo hilo kwa kuwa jambo hilo linaathiri shughuli za mipakani kwa pande zote mbili.

Bw. Simwinga alisema tayari wameshaanza kuwaeleza wananchi wao waliojenga ndani ya mpaka huo kuanza kuondoka, ambapo Waziri Mkuu amesema wanataka eneo hilo liwe wazi ili iwe rahisi kuutazama mpaka huo kwa umakini.

Mkuu huyo wa wilaya ya Nakonde alisema utekelezaji wa jambo utafanikiwa kwa urahisi kutokana na ushirikiano wa Serikali za Tanzania na Zambia.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JULAI 21, 2017

No comments:

Post a Comment

Pages