Dande Contact

TEMBELEA BLOG HII KWA MATUKIO YA KILA SIKU-MOBILE +255 713 623 958 / +255 784 623 958 EMAIL dande15us@gmail.com

Halotel


CRDB

CRDB
.

Pages

Wanafunzi 577,kikombe kimoja,maji kwa foleni

NA HAPPINESS MNALE

UPATIKANAJI wa maji safi na salama ni mojawapo ya mahitaji ya msingi kwa binadamu wote.

Suala hili linatiliwa mkazo katika malengo mahususi ya kitaifa na kimataifa ikiwemo Malengo ya Maendeleo Endelevu. 

Katika lengo la sita la maendeleo endelevu linadhamiria kuona kuna upatikanaji wa maji safi na salamakwa wote ifikapo 2030.

Nchini Tanzania, jitihada za upatikanaji wa maji safi na salama zipo katika kila hatua ya Mkakati wa Kukukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (Mkukuta).

Jitihada hizi pia zipo kwenye Dira ya Maendeleo Taifa ya mwaka 2015 (Tanzania Development Vision) na katika ilani zote za uchaguzi za vyama vya siasa. 

Yapo makubaliano ya pamoja kwamba maji ni kipaumbele cha muhimu lakini bado upatikanaji wake hasa hapa Tanzania ni mgumu.

Hivi karibuni Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) pamoja na washirika wenza wakiwemo Haki Elimu na Twaweza waliadhimisha wiki ya elimu Wilaya ya Nanyumbu Mkoa wa Mtwara.

Juma hilo lililopewa kauli mbiu ya Uwajibikaji wa Pamoja kwa Elimu Bora na Jumuishi lililenga kuukomboa Mkoa wa Mtwara kutokana na changamoto lukuki katika sekta ya elimu.

Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja ukosefu wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo.
Kati ya shule ambazo zilifikiwa ni shule ya msingi Mnanje B.

Shule hiyo iliyoanza mwaka 1979 ikiwa na wanafunzi 65 kwasasa wanafunzi 577 huku ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa matundu ya vyoo ambapo mahitaji yao ni matundu 22 na sasa wanayo sita.

Kwa matundu haya ni dhahiri kwamba hali za wanafunzi ziko shakani.

Lakini tukiachana na hilo lipo kubwa zaidi katika shule hii ambalo linaweza kusababisha wanafunzi wengi kutokufika shule kwasababu ya kuugua.

Nikiwa katika shule msingi Mnanje B nilishuhudia kengele ikigongwa na ndipo nikaona kundi kubwa la wanafunzi likikimbia na kuwahi kupanga mstari.

Nilijiuliza kulikoni, mbona mstari wenye kupambana kwa ubavu,ndipo nikasogea.

Niliona mwalimu akiwa katikati ili kuimarisha usalama na kutuliza vurugu.

Ndipo nilipoona ndoo tatu za maji, kikombe kimoja chenye rangi nyeusi kilichotumika kuchota maji hayo ambapo wanafunzi walipokezana kunywa kwa kufuata msitari huo.

Nikajiuliza kichwani, haya maji ni safi na salama? Yamechotwa wapi? Mbona sikuona mifuniko ya ndoo ikifunuliwa? Inamaana yalikuwa wazi muda wote?
Nikajiuliza tena mikono ya wanafunzi ni salama kuingiza katika ndoo zile na kunywa maji huku akimuachia mwenzake? Nikasema lakini mbona kikombe kinachotumika ni kimoja na msululu ni mrefu tena wakipokezana wote?

Taa nyekundu ikawaka kichwnai kwangu nikasema nikajihoji vipi kuhusu afya zao endapo mmoja atakuwa na ugonjwa ama TB, fangasi za kinywa si ataambukiza wenzake?

Niliwaona wanafunzi wale wakinywa maji kwa kupokezana nikasogea zaidi  kuchungulia maji nikayaona yakiwa hayana rangi ya kuvutia.

Nikamuuliza mwalimu haya maji yanapatikana wapi, akasema yameletwa na wananchi ambayo mengine ndio wanayofyatulia tofali.

Nikamuuliza tena mmeweka dawa ya kuua vijidudu, akasema huku dawa utapata wapi? 

Mmoja wa walimu wa shule hiyo, ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kwamba wamekuwa wamekuwa wakiwapa wanafunzi maji kutokana na uhaba wa maji katika maeneo yao.

“Tulikubaliana na wazazi kwasababu shule hii inatoa lishe mchana ili kuwavutia watoto kuacha utoro hivyo wanapata chakula, kwahiyo katika kupata chakula huwa wanakuywa maji pia,”anasema.

Mmoja wa wanafunzi hao, Mwanahawa salum, alisema kwamba maji hayo huchotwa visimani na kuwekwa kwenye mapipa ambapo inapofika saa 4:00 muda wa mapumziko hupata fursa ya kunywa maji.

Mwanafunzi mwingine Juma Habibu anasema kwamba kuna nyakati huwa anaugua tumbo lakini hajajua kama maji hayo ni chanzo.

Mmoja wa wazazi Asha Salum, anasema kwamba wazazi hulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji katika visima ama madimbwi.

“Maji yenyewe unayapata mbali na wakati mwingine machafu maana ukisubiri yale wanayosambaza hayana uhakika ndio maana tunachota kwenye visima, tunachojua kuwapa tu watoto ili wanywe, kwa usalama sijui kama salama,”anasema.

Mshauri wa afya na tiba manispaa ya Kigamboni, Dk. Fredy Mchinamnamba, anasema kwamba unywaji maji wa kupokezana kikombe unaweza kusababisha magonjwa ya kuambukiza katitika kinywa na meno pamoja nay ale ya mfumo wa hewa.

Anasema kwamba kimsingi wanafunzi wa shule za msingi ni waathirika zaidi kutokana na umri wao.
Anasema kwamba magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya hewa yanaenezwa kwa kwa kuvuta pumzi iliyo na vijidudu vya ugonjwa husika.

Dk. Mchinamnamba anasema kwamba magonjwa yanayoweza kuambukizwa kwa njia ya hewa ni kama vile surua, kifua kikuu (TB).

 Anasema pia magonjwa kama kikohozi na mafua “Lakini serikali ilishachukua hatua mbali mbali katika halmashauri mfano kuanzisha kitengo cha elimu mashuleni ambacho kimsingi kinatakiwa kiboreshwe na kiwezeshwe ili kiweze kuwafikia wanafunzi wengi mashuleni,”anasema
Lakini hali ya upatikanaji wa maji ukoje?

Tangu mwaka 2006, Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji (WSDP) unaoongoza jitihada za serikali na wadau wa maendeleo kusambaza maji salama. Ambapo zaidi ya dola bilioni 1.2 zimetumika kati ya mwaka 2013 na 2016.

Hali hii ilisababisha usambazaji wa maji kuwa kipaumbele cha sita cha awali. Taasisi ya Twaweza ilifanya utafiti wa hali ya upatikanaji wa maji kwa mwaka 2017.

Utafiti huo ulibaini kwamba asilimia 54 ya kaya za Tanzania zinapata maji kutoka katika vyanzo vilivyoboreshwa.
Lakini pia upatikanaji wa maji safi vijijini haujaongezeka kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita ambapo uchotaji maji bado ni zoezi linalochukua muda na kimsingi limebakia kuwa jukumu la wanawake na watoto.

Utafiti wa Twaweza pia ulibaini asilimia 60 ya kaya za Tanzania hutibu maji na njia kuu inayotumika ni kuyachemsha maji ingawa changamoto ya umbali wa kuyapata hasa vijijini na maji hayo kuwa machafu.

Lakini Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilionyesha kwamba upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya vijijini haujabadilika tangu mwaka 2015.

Ambapo kati ya tafiti 14, 12 kati ya hizo zilikadiria kwamba kati ya asilimia 41 na asilimia 48 ya kaya zinatumia vyanzo vilivyoboreshwa kwa ajili ya maji ya kunywa.

Hata hivyo, takwimu za Sauti za Wananchi zinanonesha kuwa upatikanaji wa maji umepungua kutoka asilimia 55 mwaka 2014 hadi asilimia 46 mwaka 2016.

Wizara ya Maji, Umwagiliaji imeripoti kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa maji kati ya asilimia 50 na asilimia 60 na takwimu za Matokeo Makubwa Sasa pia zinaripoti ongezeko la kasi kutoka asilimia 40 mwaka 2013 hadi asilimia 67 mwaka 2015.

Twaweza pia wanasema asilimia 43 ya watu wa vijijini wanapata maji ndani ya dakika 30 zilizopendekezwa katika malengo ya kitaifa ikiwemo Mkukuta. 

Lakini asilimia 19 wanatumia kati ya dakika 30 hadi 60 na asilimia 38 wanahitaji zaidi ya saa zima kupata maji.

mnaleh@yahoo.com

No comments:

Post a Comment