HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 21, 2017

TUTABORESHA HUDUMA ZA MAJI NA UMEME CHEMBA NA KONDOA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini zikiwemo wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma.

Amesema Serikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumatano, Septemba 20, 2017) alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Chemba na Kondoa waliomsimamisha katika maeneo ya Chemba, Kalema, Bicha na Bereko akiwa njianu kuelekea mkoani Arusha kwa shughuli za kikazi.

Alisema kwa sasa Serikali imeendelea na uchumbaji wa visima virefu, vifupi pamoja na kuweka mtandao wa mabomba ya kusamba maji katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo na ya wilaya hizo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo karibu na makazi yao.

Pia Waziri Mkuu alisema wananchi wanatakiwa wazingatie sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji wawachukulie hatua watu wote watakaokutwa wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa nishati ya umeme, Waziri Mkuu alisema hakuna kijiji nchini kitakachoachwa bila ya kuunganishiwa huduma hiyo katika awamu ya tatu ya Mradi wa Nishati Vijijini (REA). 

Ameagiza wakandarasi wamalize maeneo yaliyosalia katika REA awamu ya pili ndipo waendelee na awamu ya tatu. Alisema Serikali imetenga sh. trilioni moja kwa ajili ya kusambaza umeme katika vijiji 8,000 ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo.

“Rais wetu Dkt. John Magufuli anajali sana wananchi wake, hivyo ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na vya wilaya za Chemba na Kondoa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”

Pia Waziri Mkuu alisema  mwananchi hawatowajibika tena katika kulipia nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

Waziri Mkuu aliongeza kwamba  lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania na kwa vile ambavyo viko kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi vitafungiwa sola, jambo ambalo litafungua fursa za ajira na kukuza uchumi.
Awali mbunge wa Chemba, Bw. Juma Nkamia, Mbunge wa Kondoa Mjini Bw. Edwin Sanda na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji ambaye ni Mbunge wa Kondoa Vijijini waliomba Serikali iwasaidie katika kutatua kero ya maji na umeme.
Walisema katika maeneo mbalimbali ya majimbo yao wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya umeme pamoja na maji safi na salama hivyo kusababisha wananchi kushindwa kushiriki vema kwenye shughuli za kimaendeleo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
ALHAMISI, SEPTEMBA 21, 2017.
                                         

No comments:

Post a Comment

Pages