HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 13, 2017

DKT ANGELINA MABULA AAHIDI WATAALAMU WA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI SINGIDA

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeahidi kutoa timu ya wataalamu watakao suluhisha mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida na Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara.

Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara yake Mkoani Singida katika kijiji cha Singa tarafa ya Kinampundu Wilayani Mkalama ambapo amesema Wizara yake itatoa wataalamu watakaoweza kutatua mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 30.

“Kwakuwa pande zote mbili za Mkalama na Hanang’ zimekutana mara kadhaa bila mafanikio, nitaleta wataalamu wafike eneo la mpaka ili wataalam hao wawasomee alama moja baada ya nyingine, kila mmoja wenu afahamu eneo lake mwisho ni wapi, nadhani hapo tutakuwa tumewasaidia wananchi wetu”, amesema Dkt Mabula.

Amesema wananchi wa Kijiji hicho cha Singa wasiwe na wasiwasi endapo baada ya kuonyesha mpaka wao mashamba yao yakionekana yapo wilaya ya Hanang’ wataruhusiwa kuendelea kuyamiliki ila watatakiwa kwenda kujitambulisha katika Uongozi wa Wilaya hiyo.

Aidha Dkt Mabula amesema timu hiyo ya wataalamu itahakikisha inasuluhisha migogoro yote ya mipaka ya wilaya hiyo ambayo ngazi ya wilaya imeshindikana kutatuliwa.

Amewashauri wananchi hao kutouza au kugawa ardhi yao ovyo ovyo kwakuwa ardhi ni mali na mtaji popote pale hata kama ni vijijini hivyo watunze ardhi yao na kuiongezea thamani kwa kuipima na kuwa na hati ya umiliki.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walitoa malalamiko kwa Naibu Waziri huyo huku wakimueleza kuwa mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu umesababisha baadhi yao kupelekwa mahakamani kwa madai ya kuvamia mashamba.

Mzee Anaftali Amosi Majii amemueleza Naibu waziri kuwa taarifa za mgogoro huo zilitolewa muda mrefu na kuongeza kuwa wananchi wamechoka kushitakiwa kwa makosa ya uvamizi wa mashamba wakati wao wanaamini wanayamiliki kwa uhalali jambo ambalo linawachelewesha kimaendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama Mhandisi Geofrey Sanga amesema Wilaya ya Mkalama ina migogoro ya mipaka kwa wilaya tano zinazowazunguka.

Mhandisi Sanga ameeleza kuwa Mkalama ina migogoro ya mipaka kati yake na Wilaya za Mbulu, Iramba, Hanang’ na Wilaya ya Singida jambo ambalo linawafanya baadhi ya wananchi kukwepa kuchangia shughuli za maendeleo wakidai wao sio wa Wilaya hiyo.

Wakati huo huo Naibu Waziri Dkt Angelina Mabula amefanya ziara Wilaya ya Iramba na kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika masijala ya Ardhi ya Wilaya hiyo ambapo hakuridhishwa na utunzaji wa nyaraka pamoja na utendaji usioridhisha unaosababisha wananchi kuchelewa kupata hati za viwanja.

Dkt Mabula pia hakuridhishwa na kasi ndogo ya upimaji viwanja na utoaji wa hati wilayani humo huku akiwataka kuacha kukusanya kodi mbalimbali za ardhi kwa utendaji wa kimazoea bali wafanye kazi bidii.

No comments:

Post a Comment

Pages