HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 19, 2017

LIGI KUU BARA USHINDANI KILA KONA

Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), inatarajiwa kuendelea kesho Ijumaa Oktoba 20, 2017 kwa mchezo mmoja utakaokutanisha timu za Mwadui na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mwadui mkoani Shinyanga.

Timu hizo zinakutana katika Raundi ya Saba katika duru hili la kwanza la VPL ambalo mbali ya Kampuni ya Simu ya Vodacom - wadhamini wakuu, wadhamini wengine ni Kituo cha Televisheni cha Azam (Azam Tv) na Benki ya KCB ambayo huduma zake za kibenki zinazidi kushamiri nchini.

Wadhamini hao wanachagiza ligi hiyo ambayo itaendelea Jumamosi Oktoba 21 kwa michezo sita  itakayofanyika kwenye viwanja tofauti huku mechi nyingi zikipata fursa ya kuonyeshwa kwenye chaneli mbalimbali za Azam Tv kupitia king’amuzi cha Azam.

Michezo ya Jumamosi itakutanisha timu za Mbao na Azam kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wakati Lipuli itakuwa mwenyeji wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa ilihali Ruvu Shooting watakuwa wageni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Jumamosi hiyo hiyo Simba yenye mabadiliko kidogo kwenye benchi la Ufundi, itawaalika Njombe Mji kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku Ndanda ikicheza na Singida United kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Wakati Jumamosi hiyohiyo tena, Mtibwa Sugar wakicheza na Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro, Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja tu - ambao ni kati ya Stand United na mabingwa watetezi, Young Africans ya Dar es Salaam - mchezo utakaopigwa Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

No comments:

Post a Comment

Pages