HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 18, 2017

MASHINDANO YA KIWANGA JIMBO CUP 2017 YAHITIMISHWA KWA MLIMBA STAR KUTWAA UBINGWA

 Katibu Tawala wa wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Robert Selasela kushoto na Mbunge wa jimbo la Mlimba, Susan Kiwanga wakimkabidhi zawadi ya kombe nahodha wa Mlimba Star, Yusuph Kuda baada ya kuibuka mabingwa wa mchezo wa soka wa ligi ya Kiwanga Jimbo Cup 2017 kwa kuifunga bao 1-0 Mchombe FC katika fainali iliyofanyika uwanja wa Matangini kijiji cha Mlimba juzi. (Picha na ofisi ya Katibu wa Mbunge).
 Na Mwandishi Wetu
 
Mshambuliaji wa timu ya soka ya kata ya Mlimba Star FC, William Maembe ameiwezesha timu yake kutwaa ubingwa wa mashindano ya Kiwanga Jimbo Cup 2017 baada ya kufunga bao pekee dhidi ya timu ya kata ya Mchombe FC katika mchezo mkali wa fainali uliopigwa kwenye uwanja wa shule ya msingi Matangini kijiji cha Mlimba wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Katika mchezo huo ulimalizika kwa Mlimba FC kupata bao 1-0 na kufuta ndoto ya timu ya kata ya Mngeta FC kuwa mabingwa wa kwanza wa ligi hiyo huku timu ya netiboli ya tarafa ya Namawala nayo ikiitwanga timu ya tarafa ya akinadada wa Mlimba B kwa vikapu 24 kwa 23 na kutawazwa mabingwa wa mchezo huo.

Mshambuliaji huyo, Maembea alifunga bao hilo dakika ya 6 kwa kuunganisha krosi ya John George na kufungwa kwa kichwa na kukata ngebe za wapinzani wao.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha michezo ya ligi hiyo, Mbunge wa jimbo la Mlimba, Suzan Kiwanga alisema kuwa ligi ya Kiwanga Jimbo Cup 2017 imepata mabingwa wa kihistoria na kuhitimisha na kupambwa na vikundi vya burudani vya muziki wa kizazi kipya na ngoma za asili wilaya hapa.

Kiwanga alisema kuwa lengo la kuanzisha kwa ligi hiyo ni kuwaunganisha vijana kwenye kata na vijiji ili kukaa pamoja na kudumisha michezo kupitia michezo na kuonyesha vipaji vyao vya soka.
 
“Kuna vipaji vingi vya michezo ndani ya jimbo hili na tumeshuhudia vijana wakionyesha vipaji kwenye mchezo wa soka, netiboli, muziki wa kizazi kipya, ngoma za asili lakini ligi hii imehitimishwa kwa michezo mbalimbali kwa Wazee kufuta kamba na kufukuza kuku ambapo washindi wamekabidhiwa zawadi za ushindi wa kwanza.”alisema Kiwanga.

Mratibu wa ligi hiyo, Katibu wa Mbunge wa jimbo la Mlimba, Frank Magele alisema kuwa ligi hiyo iligawanywa kwenye vituo vya kata nne za tarafa za Mngeta na Mlimba ambapo timu 16 zilichuana kwa kushindana katika michezo ya awali ili kupata timu za kuingia robo fainali, nusu fainali na fainali.

Magele alisema kuwa Mlimba Star FC ilikabidhiwa zawadi ya kombe, fedha sh550,000, mipira miwili na jezi seti moja wakati mshindi wa pili timu ya Mchombe FC jezi seti moja, mipira miwili, fedha sh200,000 na mshindi Ching’anda FC iliambulia jezi seti moja, mpira mmoja na fedha sh100,000.

Kwa upande wa netiboli timu ya tarafa ya Mngeta ilikaidhiwa zawadi ya mshindi wa kwanza sh200,000, mpira mmoja na mshindi wa pili Mlimba B ilikabidhiwa sh100,000.

“Tulikuwa na mabingwa wa vituo vinne ambapo alikabidhiwa zawadi ya sh50,000 kila mmoja na kituo cha Namawala bingwa alikuwa Mofu Stars, kituo cha Mngeta alikuwa Mchombe FC, kituo cha Mlimba, Mlimba Star na kituo Utengule, Utengule United.

No comments:

Post a Comment

Pages