HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 22, 2017

Mkurugenzi TAA ataka TUGHE kutetea wafanyakazi

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela leo akiongea na baadhi ya viongozi wa Matawi ya Chama cha Wafanyakazi mahala pa kazi (TUGHE), TAA Makao Makuu na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
 Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi mahala pa Kazi (TUGHE) matawi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Makao Makuu (TAA HQ) na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), jana wakimsikiliza kwa makini Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Bw. Richard Mayongela (kushoto) alipokutana nao leo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (katikati mstari wa mbele), akinyanyua mikono juu kuashiria mshikamano daima na baadhi ya viongozi wa matawi wa chama cha wafanyakazi mahala pa kazi (TUGHE) matawi ya Makao Makuu na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), alipokutana nao leo. 
Na Mwandishi Wetu

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela amewataka viongozi wa wafanyakazi kupitia matawi mawili ya Chama cha Wafanyakazi, TAA Makao Makuu na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kutenda haki kwa kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi wote bila kubagua na kuwasilisha kwa mwajiri ili yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati.

Bw. Mayongela ametoa kauli hiyo leo wakati viongozi wa matawi hayo walipokwenda kujitambulisha ofisi kwake TAA Makao Makuu, ambapo alisisitiza kuwa wafanyakazi wa chini ndio wenye matatizo makubwa lakini wamekuwa hawasikilizwi na kutatuliwa matatizo yao kwa wakati.

“Ninashukuru uongozi mmekuja kuonana nami, ninahitaji ushirikiano wenu kama chama cha wafanyakazi, muwatumikie wafanyakazi kwa kutenda haki mkisikiliza matatizo ya kila mmoja na kufikisha sehemu husika na ninawaahidi kuwa nanyi bega kwa bega kutatua matatizo ya wafanyakazi kwani wao ndio wanafanya TAA iwepo, endapo wakifanya kazi bila manung’uniko wala makundi, mamlaka yetu itasonga mbele kwa kuwa uongozi sio kupigana vita bali tunatakiwa kujenga na kuwa kitu kimoja.” amesema Bw. Mayongela.

Hatahivyo amesema, kwa sasa yupo mbioni kuangalia namna ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupitia makusanyo yatakayotokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuongeza tija na ufanisi wa kazi, kwa kuwa inaonekana wengi wamekata tamaa kutokana na kufanya kazi nyingi na wakati mwingine kupitiliza muda wa kazi wa kawaida bila kupata stahiki yeyote.

“Kwa msaada wa Mungu nina imani atanionyesha wapi fedha zilipo na jinsi ya kuzitumia ipasavyo kwa masuala ya msingi, na ninakusudia hadi kufika Desemba mwaka huu niweze kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Watu wanafanya kazi sana lakini maslahi ni madogo, unaona kabisa jinsi mtu anavyoitumikia taasisi kwa moyo, lakini sura inaonesha jinsi alivyokata tamaa, ninaamini kwa kufanya hivi itaongeza tija na bidii ya kazi.” amesema Bw. Mayongela.

Halikadhalika, Bw. Mayongela amesema atahakikisha wafanyakazi wanapata vitendea kazi vya uhakika kulingana na kazi zao, zikiwemo bajaji, pikipiki na magari kwa ajili ya doria na kwa shughuli za uendeshaji ndani Viwanja vya Ndege.

Pia amewataka viongozi hao kuwa karibu na wafanyakazi ili kuhakikisha wanawahamasisha wanafanya kazi kwa bidii, uaminifu na uadilifu ili kuondoa mianya na tabia za upokeaji wa rushwa, kwa kuwa TUGHE ni daraja kati ya mwajiri na wafanyakazi.

Naye Mwenyekiti wa TUGHE tawi la TAA Makao Makuu, Bw. Nasib Elias mbali na kumshukuru Kaimu Mkurugenzi Mkuu kwa kuwapa fursa ya kukutana naye, lakini amemuomba kuendelea kudumisha mahusiano baina ya mwajiri na chama cha wafanyakazi (TUGHE), na pia kumuomba aitake menejimenti yake kuwa na utaratibu wa kuweka milango wazi kwa wafanyakazi kama yeye ili waweze kusikiliza na kutoa majibu sahihi kwa baadhi ya masuala ya kiofisi yanayowasilishwa na wafanyakazi kwao na sio kila jambo liwasilishwe kwake.


“Tunakuombea kwa Mungu akutie nguvu kwa haya unayotaka kufanya likiwemo la kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kuwa litasaidia kuamsha morali ya kazi kwa wafanyakazi, lakini hii sera yako ya kuwacha milango wazi tunaomba nayo itekelezwe katika ngazi ya menejimenti yako kwani kuna mambo ambayo yanaweza kumalizwa na Wakurugenzi na Mameneja wenyewe na sio lazima yafike kwako, “ amesema Bw. Elias.

Katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi ambacho kimeonekana ni kipaumbele cha Kaimu Mkurugenzi mkuu kwa wafanyakazi, Bw. Elias amemuomba kuangalia namna bora ya kusimamia maslahi hayo ikiwemo kuuasili mkataba wa hali bora (SBA) kama inavyotekelezwa na taasisi nyingine za serikali.

No comments:

Post a Comment

Pages