HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 21, 2017

NAIBU WAZIRI AKABIDHI MSAADA WA MABATI KWA SHULE ILIYOATHIRIKA NA KIMBUNGA

Na Hamza Temba-Wizara ya Maliasili na Utalii

 Katika jiihada za Serikali za kuendeleza ushirikiano na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa msaada wa mabati sitini kwa ajili ya kuezeka madarasa ya shule ya msingi Kipanga baada ya kuezuliwa na kimbunga hivi karibuni katika kijiji cha Ubwachana Wilaya ya Iringa mkoani Iringa.

Msaada huo umetolewa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga alipotembelea kituo cha Malikale cha Isimila mkoani humo ambacho kinapakana na shule hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Mkoani humo.

Akikabidhi mabati hayo, Naibu Waziri Hasunga alisema  Serikali inatambua mchango wa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi kwenye uhifadhi shirikishi hivyo ni jukumu la Serikali kuwaunga mkono pale wanapopatwa na majanga ya aina mbalimbali.

Aidha, aliwataka baadhi ya wananchi wanaochimba mchanga kwenye maeneo ya vivutio katika kituo hicho waache mara moja kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria kwakuwa wanahatarisha uhai wa kingo za miamba ya kale ambayo na kivutio kikubwa cha utalii wa asili katika ukanda wa kusini.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya mambo ya Kale wa Wizara hiyo, Bi. Digna Tillya alitoa rai kwa wananchi wanaozunguka kituo hicho kushirikiana na Serikali katika uhifadhi na ulinzi wa kituo hicho na kujiepusha na vitendo vya uharibifu wa mazingira.

No comments:

Post a Comment

Pages