HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 16, 2017

SERIKALI KUANZISHA TAASISI YA ITAKAYOSIMAMIA USALAMA BARABARANI

MWANDISHI WETU

SERIKALI imesema ipo katika mchakato wa kuanzisha taasisi kiongozi ambayo itakuwa inasimamia usalama barabarani huku ikiendelea kufanya maboresho katika Baraza la Usalama Barabarani.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Wadau wa Sekta ya Barabara Tanzania (Tara) jana jijini Dar es Salaam.

Nyamhanga alisema Serikali imefikia uamuzi huo kutokana na ukweli kuwa kumekuwepo na ongezeko la ajali za barabarani hivyo kuwepo kwa taasisi ambayo itasimamia usalama barabarani inaweza kuwa njia rahisi ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Katibu mkuu huyo alisema taasisi kiongozi itakuwa inataribu na kusimamia masuala yote ya usalama barabarani kama kuhakikisha elimu inatolea, ubora wa barabara na kusimamiwa kwa sheria.

Alisema pia taasisi hiyo itakuwa inasimamia uokoaji wakati wa ajali hali ambayo itakuwa ni picha nzuri katika utatuzi wa sekta hiyo.

“Nawapondeza Tara kwa kuaamua kukutana na kujadiliana kuhusu masuala ya usalama barabarani na katika kuwaunga mkono Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha taasisi kiongozi ambayo itaratibu masuala yote ya barabara,” alisema.

Alisema upitia taasisi hiyo watahakikisha kuwa hata taratibu za kupata leseni na sifa za dereva zinapita katika mkondo sahihi.

Aidha, alisema wakati mchakato wa kuanzisha taasisi hiyo kiongozi watakuwa wanatumia baraza la usalama barabarani kufuatilia masuala yote ya barabara kwa kushirikiana na vyombo vilivyopo kama polisi na vinginevyo.

Nyamhanga alisema kinachofanyika kwa sasa ni kuimarisha baraza hilo kwa kulipatia mahitaji yote muhimu huku mchakato wa kuanzisha chombo kipya ukiendelea.

Akizungumza kabla ya ufunguzi wa mkutano huo Mwenyekiti wa Tara, Mhandisi Abdu Awadhi aliitaka Serikali kutekeleza mapendekezo ambayo wajumbe wa taasisi hiyo wamekuwa wakiyatoa katika kuboresha usalama wa barabarani.

Awadhi alisema Tara imekuwa ikifuatilia usalama wa barabara kwa zaidi ya miaka 20 lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanaotumia kuwa salama.

“Tara ni taasisi ambayo inafanya kazi na Serikali hasa katika sekta ya barabara, jeshi la polisi na wengine wengi ambao pamoja ni kuhakikisha barabara zinakuwa bora,” alisema.

Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa Watanzania kujiunga na taasisi hiyo ili kwa pamoja waweze kupigania ubora wa barabara.

Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Fortonatus Muslimu aliwataka madereva kufuata sheria za usalama barabarani kwani jeshi hilo halitamvumilia mtu yoyote anayetebda makosa.

Alisema hivi karibuni wamekamata madereva wa mabasi saba eneo la Kibaha mkoani Pwani na saba mkoani Simiyu ambao walikuwa wanaendesha kwa mwendokasi nyakati za usiku na kwamba wapo mahabusi kusubiri kufikishwa mahakamani.

Muslimu alisema iwapo madereva hao watakutwa na makosa mahakamani wanatarajia kuwanyang’anya leseni ili waache kazi hiyo na kufanya kazi nyingine.

“Dereva ambaye atafikishwa mahakamani na kukutwa na hatia nitamfutia leseni ili aende kufanya kazi nyingine kwani udereva umemshinda,” alisema.

Aidha, Muslimu alisema changamoto kubwa ambayo wanapambana nayo ni wananchi na madereva kutofuata sheria za barabarani hasa kwenye vivuko, ulevi, mwendokasi, kung’olewa kwa alama za barabarani.

Alisema ni jukumu la kila mwananchi kutumia nafasi yake kutoa taarifa katika jeshi la polisi pale ambapo anapoona ukiukwaji wa sheria za barabarani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Usalama Brabarani kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania, Jotelam Kibatele aliomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwepo vyombo vya usafiri ambavyo ni rafiki kwa kundi hilo. Aidha, Kibatele alisema changamoto nyingine ni kmadereva kushindwa kutii alama za barabarani hasa za kundi la watu wenye ulemavu hali ambayo ni hatari kwao.

No comments:

Post a Comment

Pages