HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 23, 2017

TPB Bank Plc, Multichoice kuwapatia Watanzania DStv kwa Mkopo

BENKI ya TPB imeingia kwenye makubaliano rasmi na kampuni ya Multichoice Tanzania inayotoa huduma za DStv ambapo wafanyakazi umma, wateja na hata wale wasio wateja sasa wanaweza kupata ving’amuzi vya DStv kwa mkopo na kisha kulipia kidogo kidogo.
 
Hafla hiyo ya kusaini makubaliano imefanyika leo jijini Dar es Salaam, ambapo Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya TPB Sabasaba Moshingi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande wamesaini hazi za makubaliano.
 
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Sabasaba Moshingi alisema kwa sasa Watanzania wanaotaka kumiliki ving’amuzi vya DStv, wataweza kupata mkopo maalum kutoka TPB utakaowawezesha kufungiwa huduma za DStv na kisha kulipa kwa awamu kwa kati ya miezi mitatu hadi mwaka mmoja.

Alisema kuwa benki yake siku zote imekuwa ikijitahidi kubuni huduma mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kupata huduma muhimu na pia katika kuboresha hali zao kiuchumi na kijamii.
 
Amesema kuwa wameamua kuingia kwenye makubaliano na kampuni ya Multichoice ili kuwapa fursa wafanyakazi na wateja wa benki hiyo waweze kupata huduma muhimu za DStv kwa mkopo, hii ikimaanisha hawatalazimika kulipa fedha yote kwa mkupuo mmoja badala yake watakuwa wanalipa kwa awamu kadhaa.
 
“Benki yetu ni benki ya Watanzania wa kada zote, na wenzetu wa Multichoice nao hali kadhalika, sasa tumeamua tuungane ili tuwawezeshe ndugu zetu Watanzania kupata fursa ya kuwa na huduma ya DStv kwa njia ambayo ni rahisi kwao” alisema Moshingi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Maharage Chande aliishukuru TPB kwa kukubali kuwawezesha watanzania kupata huduma za DStv kihimiza wananchi kuitumia vema fursa hiyo. Alisema huduma za ving’amuzi vya DStv ni bora nchini Tanzania hivyo urahisishaji wa wananchi kuipata unaongeza wingo wa wananchi kufurahia huduma hizo.

No comments:

Post a Comment

Pages