HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 11, 2017

MABUNGEYA AFIKA MASHARIKI YATAKIWA KUTENGA BAJETI ZA MICHEZ0

MABUNGE ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yametakiwa kutenga bajeti za michezo za kutosha ili kuongeza ufanisi wa mashindano ya mabunge hayo yanayofanyika kila mwaka.

Kauli hiyo ya kuzitaka nchi hizo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakiyembe wakati akifunga mashindano ya nane ya michezo ya mabunge hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema amepata taarifa kuhusu bajeti hivyo ni matumaini yake kuwa katika mashindano yajayo changamoto hiyo haitakuwepo.

Dk.Mwakiyembe alisema ni jukumu la mabunge kutenga bajeti nzuri kwa ajili ya michezo ili kuhakikisha kuwa yanashiriki bila hofu yoyote katika mashindano mbalimbali.

Waziri alisema iwapo mabunge yatatenga bajeti inayotosheleza ni dhahiri kuwa ushindani utakuwepo wakati wa mashindano .

"Hamjasema katika risala yenu kuhusu ufinyu wa bajeti lakini najya bajeti zenu ni ndogo sana nadhani wakati umefika kwa kuwepo bajeti ya kutosha ya michezo ili kuleta ufanisi," alisema.

Aidha, alitoa rai kwa bunge kutumia wizara ya michezo ili kuweza kuweka mazingira rafiki ya kuhakikisha ushiriki mkubwa wa wananchi katika mashindano hayo kwa miaka ijayo.

Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Ackson alisema mashindano hayo yanapaswa kutumika kudumisha mshikamano, umoja na ushirikiano baina ya nchi zao na wananchi.

Dk.Ackson alisema katika mashindano hayo ya nane ambayo yalishirikisha zaidi ya wabunge na watumishi 800 kutoka nchi za Burundi, Uganda, Kenya, Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na Tanzania yalifana pamoja na changamoto kidogo zilizotokea.

Alisema mashindano hayo yanapaswa kuwa endelevu kwani yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza umoja, ushirikiano na mshikamano kati ya nchi wanachama.

"Mashindano haya yalianza Desemba mosi na yamemalizika jana kwa mafanikio makubwa sana naamini mashindano ya mwakani ambayo yatafanyika nchini Uganda yataboreshwa zaidi," alisema.

Naibu Spika alisema ni imani yake kuwa mashindano yajayo yatarekebisha kasoro ambazo zimejitokeza hasa katika mchezo wa pete ambapo kulikuwa na mgogoro kidogo.

Alisema katika mashindano hayo michezo saba ilichezwa ambayo ni gofu, riadha, pete, wavu, mpira wa miguu, kuvuta kamba na kutembea kwa kasi.

Dk.Ackson alisema Bunge la Tanzania limefanikiwa kuibuka na vikombe vitatu ambavyo ni vya kuvuta kamba, kutembea kwa kasi na mbio za kupokezana vijiti wanawake.

"Uganda wamepata vikombe katika mpira wa miguu, wavu wanawake na gofu huku Kenya wakibuka videdea katika riadha wanaume na wanawake, wavu wanaume na Burundi wakipata tuzo ya timu bora," alisema.

Mwenyekiti wa Bunge Sports Club, William Ngeleja alishukuru Bunge la Tanzania kufanikisha mashindano hayo kwa ufanisi na usalama wa kutosha na kwamba sasa wanajiandaa na mashindano ya mwakani.

Ngeleja alisema ni matarajio yake kuwa changamoto zilizojitokeza zitafayiwa kazi kwenye mashindano mengine ya mwakani.

No comments:

Post a Comment

Pages