HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 11, 2017

SERIKALI YASAINI MIKATABA YA BILIONI 702

SERIKALI imesaini mikataba minne na kampuni nne za ujenzi wa barabara yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 702 kwa ujenzi wa kilomita 402.

Tukio hilo kusaini mkataba hiyo limeshughudiwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, Mwakilishi Makazi wa Benki ya Mandeleo Afrika (ADB), Hellen Minja, wabunge ambao barabara zitajenfwa, wawakilishi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na wakandarasi walioshinda zabuni.

Akizungumzia utiaji saini huo Waziri Mbarawa alisema fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa barabara kutoka Tabora, Usesula hadi Mpanda Katavi kilomita 335 na kilomita 67 kutoka Mbinga hadi Mbamba Bay mkoani Ruvuma.

Mbarawa alisema ujenzi wa barabara hizo ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na ahadi za Rais John Magufuli wakati wa kampeni.

Alisema fedha hizo zimetolewa na ADB ikiwa ni baada ya serikali kuomba msaada mwaka 2015 ili kuweza kufungua fursa zilizopo katika maeneo husika kwa miradi.

Waziri alitumia nafasi hiyo kuwataka wakandarasi walioshinda zabuni kujenga barabara zenye ubora na viwango kwa kuzingatia muda wa ujenzi.

Mbarawa alisema nia ya serikali ni kuona ujenzi wa barabara hiyo unakamilika kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

"Naomba Tanroads msimamie ujenzi wa barabara yenye ubora kwani wakandarasi wengi ni wajanja na ikitokea mtu ameharibu asipewe nafasi kabisa ya ujenzi wa barabara hapa nchini," alisema.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale alisema wakandarasi waliopewa kazi wametokana na uchambuzi mkubwa uliofanyika kati ya wakandarasi 129 waliojitokeza mwaka 2016.

Alisema ili kurahisisha ujenzi wa barabara hizo wamegawa kwa wakandarasi wanne ambapo barabara ya Usesula hadi Komanga kilomita 108 itajengwa na Kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering Group Corporation Limited ya China kwa gharama ya zaidi ya  Sh.Bilioni 158 na itajengwa kwa miezi 36.

"Komanga hadi Kasinde kilomita 108 itajengwa na Mkandarasi Kampuni ya China Wu Yi Co. Limited kwa zaidi ya sh.billioni 140 na Kasinde hadi Mpanda kilomita 105 Mkandarasi Kampuni ya China Railway Seventh Group Co.Ltd kwa sh. Bilioni 133," alisema.

Mfugale alisema barabara ya Mbinga hadi Mbamba Bay kilomita 67  inajengwa na Mkandarasi China Henan International Corporation Group Co.Ltd (Chico) kwa sh. Bilioni 129.

Alisema Tanroads imejipanga kusimamia ujenzi huo kwa kufuata viwango vinavyohitajika vya ujenzi wa barabara nchini.

Mwakilishi Mkazi wa ADB, Minja alisema ofisi yake itaendelea kutoa mchango kwa serikali katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini pale watakapo hitajika.

Minja alisema matarajio ya ADB nikuona Tanzania inapata maendeleo kwa haraka na njia rahisi ni kupitia miundombinu.

Waziri wa Majj na Umwagiliaji Mhandisi Azack Kamwele ambaye barabara ya Tabora hadi Mpanda inapita jimboni kwake alisema ujenzi huo utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya ambaye pia ni Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji alisema barabara hiyo itakuwa kiungo muhimu kati ya Tanzania, Msumbiji na Malawi.

Alisema Nyasa ina vivutio vingi vya utalii hivyo ujio wa barabara hizo utakuwa njia rahisi ya kuwafikisha watalii eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

Pages