NA JANETH JOVIN
MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kumbusho
Dawson ambaye alitoa taarifa kuhusu hosteli mpya za chuo hicho kuwa na
nyufa, amesema kwa sasa anaishi kwa hofu kutokana na kufatiliwa na watu
wasiojulikana.
Dawson amesema Januari 18 mwaka huu alianza kufatiliwa na watu asiyowafahamu ambao anadai kuwa wanataka kumteka.
Akizungumza jijini Dar es Salaam,
Dawson alisema tangu hali hiyo itokee amekuwa akiishi kwa hofu hali
inayomfanya ashindwe kwenda sehemu yoyote.
Alisema hali hiyo imemuathiri hata kimasomo kwani kwa sasa
hawezi kuhudhuria vipindi vya usiku chuoni kutokana na kuhofia kukamatwa
na watu wabaya.
"Tangu tukio hilo la kutaka kukamatwa na watu nisiyowajua
nimekuwa nikiishi kwa hofu na shida sana, hali hii inanifanya nashindwa
kutembea muda wote nakaa ndani au nikitaka kutoka lazima niambatane na
watu watatu au wanne.
Kutokana na hali hii nashindwa kusoma vizuri nimekuwa
naishi kama mkimbizi katika nchi yangu sijui hawa watu wanaonitafuta
wanania gani na mimi naomba wanipe uhuru wa kukaa katika nchi yangu
waniache nisome ili baadae nije kuisaidia nchi yangu,"alisema.
Aidha Dawson alisema anaviomba vyombo vya dola kumlinda
kwani ameshatoa taarifa Polisi na katika vyombo vyote vya ulinzi na
usalama.
"Mimi ni raia wa Tanzania na kwa mujibu wa katiba ya nchi
nina haki ya kulindwa hivyo naviomba vyombo vya dola kunilinda na
kuwakamata watu hao ambao ni wa halifu, "alisema.
Picha za nyufa hizo zilianza kusambaa Desemba 3 mwaka jana
ambapo zilikuwa zikionyesha nyufa katika majengo hayo yaliyozinduliwa na
Rais John Magufuli Aprili 15, 2017.
Ujenzi wa hosteli hizo ulifanywa na Wakala wa Majengo (TBA) kwa muda wa miezi minne na kugharimu Bilioni 10.
No comments:
Post a Comment