HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 23, 2018

Mwenyekiti HUSEA kuongoza Wataalam Mipango Miji

Na Mwandishi Wetu

Wataalam wa Mipango Miji na Vijiji nchini wameunda Umoja wao na kumchagua, Renny Chiwa, kuwa mwenyekiti wa kwanza wa umoja huo.

Chiwa (pichani), Mwenyekiti wa Kampuni maarufu ya Human Settlements Action (HUSEA), inayojihusisha na mipango miji na vijiji na inayotoa ushauri elekezi kuhusu masuala yahusuyo ardhi, alichaguliwa juzi kuongoza umoja huo.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam na ambao upigaji kura wake ulitumia teknolojia ya kimtandao, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Henry Evarist, alimtangaza Chiwa kuwa Mwenyekiti kwa kupata ushindi wa asilimia 54.9 wa kura zote zilizopigwa.

Katika uchaguzi huo, washindani wengi waliopendekezwa kupigiwa kura walikuwa ni viongozi wakuu wa makampuni mbalimbali ya mipango miji na vijiji nchini.

Chiwa alifuatiwa kwa mbali na Dr. Juma Matindana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya City Consultants,  aliyepata asilimia 21.5 ya kura zote. 

Katika hotuba yake aliyoitoa jana, ikiwa na kichwa "nimekubali" Chiwa alisema amekubali kuongoza umoja huo kwa moyo mkunjufu na atahakikisha unakuwa kiunganishi na sauti kuu ya wataalam wote wa mipango miji na vijiji.

Aliongeza kuwa yupo tayari kuufanya umoja huo kuwa chachu ya kuboresha sekta ya mipango miji na kukidhi kikamilifu mahitaji ya nchi na malengo ya serikali.

"Kwa pamoja, tuna wajibu wa kufuta dhana iliyoenea katika jamii kuwa sisi wataalam wa mipango miji ni wababaishaji, vishoka na matapeli

nitahakikisha umoja huu unafuta sifa hiyo mbaya kwa kusimamia weledi na maadili ya kazi zetu na kwa kuitetea taaluma yetu" alisema Chiwa. 

Alisema anazijua kwa kina changamoto nyingi zinazoikabili sekta hiyo na atahakikisha wanashirikiana na serikali na wadau mbalimbali katika kuinyanyua sekta hiyo ambayo bado ipo nyuma katika kuyafikia malengo ya kitaifa ya kupanga miji. 

Takwimu za hivi karibuni za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinaonyesha kuwa takribani asilimia 85 ya ardhi yote nchini haijapangwa wala kupimwa, huku wananchi wengi, hususani wa mijini, wakiwa wanaishi kwenye makazi holela.

Katika Jiji la Dar es Salaam pekee  inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wanaishi katika makazi holela.

"Tunakwenda kuishauri, kuishawishi na kuisadia serikali kufanya mapitio ya Sheria Na 8 ya Mipango Miji ya mwaka 2007 pamoja na kuiomba itoe Kanuni zake ili tupate muongozo bora na ulio bayana zaidi katika kusukuma mbele sekta hii ya mipango miji

Hii ni pamoja na kuutambua Umoja huu muhimu katika sheria hiyo au kanuni zake" alisema Chiwa ambaye kampuni yake ya HUSEA imejipatia umaarufu mkubwa kwa kuwa msitari wa mbele katika kutekeleza miradi ya urasimishaji makazi,  ikishirikiana na halmashauri mbalimbali nchini zikiwemo za Jiji la Dar es Salaam.

Wataalam wengine walioingizwa kwenye kinyang'anyiro cha  uenyekiti wa umoja huo ni pamoja na Epiphania Ibrahim, Amos Emmanuel, Deborah Ngolle na Clemence Mero.

Aidha,  katika uchaguzi huo, Dr. Clara Kweka, alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa  kupata asilimia 50, huku Irinda Marwa akishinda ukatibu mkuu kwa kupata asilimia 40.6 ya kura zote zilizopigwa.

Katika nafasi ya Katibu Msaidizi, Deogratias Mashimbi, alishinda kwa kupata asilimia 38, huku, Kusenha Dickson, akishinda nafasi ya Mweka Hazina kwa kupata asilimia 37.5 ya kura zote.

Umoja huo mpya wa Wataalam wa Mipango Miji na Vijiji, unajumuisha wataalam huru wa sekta hiyo, wakiwemo wakuu wa idara na maafisa ardhi na mipango miji, wanaofanya kazi katika halmashauri na ofisi mbalimbali za serikali, taasisi,  vyuo na makampuni binafsi.

No comments:

Post a Comment

Pages