HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 17, 2018

WAZIRI MKUU ATATUA MGOGORO WA MIAKA MITATU

*Ni wa ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara ambao umedumu kwa miaka mitatu.
Ametoa uamuzi huo leo (Jumatano, Januari 17, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime pamoja na Halmashauri ya Mji wa Tarime.
Amesema amesitisha mpango huo wa ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo kwa kuwa imepangwa kujenga katika eneo ambalo lipo mbali na wananchi.
 “Ninazo taarifa kuwa mnataka kujenga katika eneo ambalo litaigharimu Serikali kutumia fedha nyingi kwa ajili ya fidia na pia lipo mbali na makazi ya wananchi.”
Pia Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kuruhusu ujenzi huo ufanyike katika eneo ambalo ni mbali ya makazi ya wananchi kwa kuwa watashindwa kufuata huduma.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali itapeleka wataalamu watakaofanya uchunguzi na bainisha eneo sahihi la kujenga Halmashauri hiyo kwa kutumia ramani.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma kutotamani fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali ajili ya miradi ya maendeleo.

Amesisitiza kwamba wasipokuwa makini na fedha hizo zitasababisha wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini. ”Je mpo tayari kuchukuliwa hatua.?

Amesema Serikali inapeleka fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo ya wananchi na si kuwanufaisha watu binafsi.

Pia amewataka watumishi kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wawe wabunifu na wajue halmashauri zao zinahitaji nini ili kuweza kusonga mbele kimaendeleo.
Waziri Mkuu ambaye leo ameendelea na ziara yake Mkoani Mara kwa kutembelea wilaya ya Tarime  ambapo baada ya kuzungumza na watumishi alikagua hopitali ya Tarime na kuweka jiwe la msingi katika kituo cha afya cha Sirari.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, JANUARI 17, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages