HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 07, 2018

500 kupata mafunzo ya kilimo cha Papai

ZAIDI ya wanachama 500 wa Mtandao wa Kijani Kibichi Tanzania (Mkikita), wanatarajiwa kushiriki mafunzo maalum ya kufungua msimu wa kilimo cha Papai salama.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mkikita, Adam Ngamange jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Ngamange alisema mafunzo hayo yatafanyika Februari 24 mwaka huu yatabeba ujumbe 'Papai salama open speech' kwa lengo la kuunganisha walaji, wazalishaji na wataalam wa kilimo hicho.

Alisema baada ya tafiti kufanyika wamegundua mkanganyiko mkubwa wa taarifa hivyo kupitia mafunzo hayo ni wazi mabadiliko katika kilimo cha Papai yatatokea.

"Tafiti zinaonesha watalaam wanatofautiana kwenye idadi ya miche, uchimbaji wa mashimo, umwagiliaji maji na utiaji mbolea hivyo mafunzo haya yataweka washiriki kwenye mstari ili kukidhi ubora na ulinganifu wa soko la ndani na nje," alisema.

Mkurugenzi huyo alisema mafunzo hayo yatawakutanisha wabobezi na watendaji mbalimbali katika kilimo hicho kipya cha Papai salama yatakuwa  na awamu tatu tofauti ili kujenga misingi imara katika kuleta unafuu wa uzalishaji papai.

Alisema Mkikita imejipanga kikamilifu katika kuhakikisha wakulima wa Tanzania hasa wanaolima papai, mchaichai, mhogo na pilipili kichaa.

Aidha, Ngamange alisema pamoja na mafunzo hayo wanatarajia kupokea ugeni kutoka nchini Uturuki kutambua fursa za zao la papai nchini.

Pia alisema wanachama wa Mkikita wanatarajia kufanya ziara ya mafunzo Nchini Israel kuanzia Machi 11 mwaka huu na kugharimu dola za Marekani 2,000.

Halikadhalika Mkikita imesaini makubaliano ya ushirikiano  na Taasisi ya Hope For All ambayo ina wanachama zaidi ya 5,000 ili waweze kushirikiana kwenye nyanja za teknolojia na kilimo.

Akizungumzia makubaliano hayo Mkurugenzi wa Hope For All Edgar Mwamfupe alisema matarajio yao ni kuona mkulima anaheshima katika jamii.

Mwamfupe alisema kupitia Mkikita wanachama wao watafikia kwenye umilionea kwa kuwa kuna fursa za soko na biashara.

No comments:

Post a Comment

Pages