HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 25, 2018

MJUMITA YAITAKA SERIKALI KUDHITIBI UPOTEVU WA MISITU

NA SULEIMAN KASEI
MTANDAO wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) umetoa mapendekezo manne kwa Serikali ili kuhakikisha kuwa upotevu wa misitu nchini unadhibitiwa.
Mapendekezo hayo yametolewa na Ofisa Uraghibishaji wa Miradi Mjumita, Elida Fundi wakati akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari mbalimbali hivi karibuni mwishoni mwa wiki.
Fundi alitaja pendekezo la kwanza ni kuandaa sera ambazo zitatambua thamani ya huduma ya mifumoikolojia na mazao ya misitu, hasa inayohusu maamuzi na mgawanyo wa ardhi.
Alisema pendekezo lingine ni kupitia sera ili kuweka uhusiano wa moja kwa moja wa biashara,  misitu na malengo ya kusimamia ardhi yenye misitu.
“Pia sera iunge mkono miradi inayotokana na misitu (mbao, mkaa) ambayo inanufaisha jamii ili kutoa motisha kwa usimamizi endelevu wa misitu ya asili; na kufikia mahitaji ya kiuchumi ya mazao ya misitu,” alisema.
Ofisa huyo alisema wakati umefika kupitia kanuni ili mazao ya misitu ambayo yamevunwa bila kanuni za usimamizi endelevu yasihalalishwe kwenye vituo vya ukaguzi.
Aidha Fundi alisema visababishi vikuu vya upotevu wa misitu upotevu mkubwa wa misitu nchini unasababishwa na mahitaji makubwa ya ardhi kwa ajili ya kilimo ambapo taarifa ya Naforma ya mwaka 2015 takribani hekta 372,816 ya misitu hupotea kila mwaka na wakati huo huo taarifa ya Serikali ya Takwimu zasingi za Hewa Ukaa ya mwaka 2016 inaonyesha hekta 469,000 ya misitu hupotea kila mwaka.
“Taarifa zote mbili zinaonyesha kwamba upotevu huo umesababishwa ufunguaji wa mashamba kwa ajili ya kilimo,”aliongeza.
Ofisa huyo alisema tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kwamba kati ya asilimia 70 mpaka 80   ya matukio yaliyosababisha upotevu wa misitu nchini ni ufyekaji wa misitu kwa ajili ya upanuzi wa mashamba (Kilimo).
Alisema sera zilizopo hazijaweza kutoa muongozo wa namna ya  kutatua kisababishi kikuu cha upotevu wa misitu nchini akitolea mfano sera ya msitu haina tamko la  la sera linalozuia kubadilisha eneo la misitu kuwa shamba la kilimo, hususani maeneo muhimu ya kiikolojia kwa kuboresha uratibu na wizara ya kilimo, wizara ya ardhi.
Ofisa Uraghibishaji huyo alisema sera za kilimo zimekuwa zikihimiza kilimo kikubwa na kidogo bila  kuzingatia upotevu wa misitu ya asili na haitoi fursa kwa jamii na watu binafsi kuanzisha miradi inayotokana na misitu ya asili iliyosimamiwa kwa uendelevu, ingawa uchumi wa taifa unahitaji mazao yanayotokana na misitu.
Fundi alisema miradi inayosimamiwa na wananchi ingeleta motisha kwa jamii na watu binafsi ili wachague kuhifadhi misitu ya asili kwenye ardhi zao na kusimamia misitu hiyo kutokana na kanuni za usimamizi endelevu.
Alisema upotevu wa misitu umekuwa ukitokea zaidi katika ardhi za vijiji kwa asilimia ( 45.7 na endapo kiwango cha sasa cha uharibifu wa misitu kwenye ardhi ya vijiji kitaendelea mpaka kufikia mwaka 2061 hakutakuwepo na misitu kwenye ardhi za vijijiji.
Kwa upande wake Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG), Bettie Luwuge alisema pamoja na kuwepo kwa sera nzuri ni jukumu la Serikali kutenga kutengeneza maeneo madogo ya usimamizi wa mkaa ndani ya misitu katika hifadhi za vijiji kwa ajili ya uzalishaji wa mkaa endelevu.
Alisema TFCG, Mjumita na Shirika la Kuendeleza Nishati Tanzania (TaTEDO) kwa  ufadhili Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswiss  (SDC) wamedhamiria kupigania utunzaji wa misitu na mazingira kupitia Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS ) hivyo Serikali inapaswa kuunga mkono.

No comments:

Post a Comment

Pages