HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 09, 2018

SERIKALI YAFANIKIWA KUREJESHA MALI ZA NCU, SHIRECU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kurejesha mali tisa kati ya 10 za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU) ambazo zilichukuliwa kinyume cha taratibu na kuagiza watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria.

Amesema mali moja iliyobakia bado inafanyiwa uchunguzi na mali mbili za Chama Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU) nazo pia zimepatikana lakini bado ziko kwenye hatua ya makabidhiano.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.

Waziri Mkuu amezitaja mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU) zilizorejeshwa kuwa jengo la Nyanza Cooperative Union (1984) Ltd. maarufu kwa jina la “Transport House” au KAUMA House, lililopo katika kiwanja namba 242, Kitalu T, Mtaa wa Stesheni; kiwanda cha kusindika mafuta cha New Era Oil Mill, kilichopo katika eneo la Igogo; na jengo na viwanja vya Ashock Industries vilivyopo eneo la viwanda Igogo.

Nyingine ni majengo ya kilichokuwa kiwanda cha mkonge na dengu kilichopo eneo la Igogo kwenye kiwanja namba 41 na 79; jengo lililopo katika kiwanja kilichopo Isamilo namba 80, kitalu “D”; jengo lililopo katika kiwanja kilichopo Isamilo namba 110, kitalu “D” na ghala moja katika kiwanja namba 104, kitalu “A” kilichopo eneo la Igogo.

“Mali nyingine zilizorejeshwa ni jengo moja lililopo mjini Geita katika kiwanja namba 8 Kitalu “K”; jengo moja lililopo mjini Geita, katika kiwanja namba 24, Kitalu “K” na jengo lililopo Isamilo katika kiwanja namba 89 Kitalu “D”,” amesema Waziri Mkuu.

Kwa upande wa mali za SHIRECU, Waziri Mkuu amezitaja mali zilizopo kwenye hatua ya makabidhiano kuwa ni ghala lililopo Kurasini, Dar es Salaam na nyumba ya ghorofa tatu iliyopo kiwanja namba 1001 “BB” Ilala, jijini Dar es Salaam.

“Katika kusimamia misingi ya utawala bora na uwajibikaji wa watendaji wa vyama vya ushirika, Serikali inaendelea kufanya uchunguzi maalum kuhusu mikataba mibovu ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza (NCU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Shinyanga (SHIRECU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU). Vilevile, tunachunguza kushikiliwa kwa mali za ushirika bila kufuata utaratibu,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kuviamsha vyama vya ushirika vya msingi na vyama vikuu vilivyosinzia katika mikoa yote ili kujenga ushirika imara na kwamba juhudi na hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali, zinalenga kuongeza imani, hamasa na uzalishaji wa mazao na kusimamia masoko yake, na hivyo, kuinua kipato cha wakulima sambamba na kuwapatia fursa ya kujiajiri wenyewe katika sekta ya kilimo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
IJUMAA, FEBRUARI 9, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages