HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 10, 2018

USALAMA WA CHAKULA UMEIMARIKA NCHINI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hali ya usalama wa chakula nchini imeimarika kutokana na uzalishaji mzuri wa mazao ya chakula.

Aliyasema hayo jana (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.

Waziri Mkuu alitaja mazao hayo kuwa  ni pamoja na mahindi yaliyovunwa katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Katavi, Kigoma, Mbeya, Songwe na Rukwa.

“Matarajio yetu kuwa hali ya mavuno msimu huu itakuwa nzuri kwa sababu mwenendo wa unyeshaji wa mvua za vuli ulikuwa wa kuridhisha katika maeneo mengi nchini.”

Alisema Serikali inaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa hali ya utengamano na usalama wa chakula unaendelea kuwa imara kwa wananchi wote na kwa wakati wote.

Waziri Mkuu alisema Serikali inawezesha wafanyabiashara wa mazao ya chakula kuendelea kusafirisha na kuuza mazao ya chakula nje na ndani ya nchi.

Hivyo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakulima waendelee kuzitumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda mazao stahiki na kutumia chakula walichonacho kwa uangalifu hadi msimu mwingine wa mavuno.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema upatikanaji na usambazaji wa pembejeo kwa wakulima umeimarika, ambapo takwimu zinaonesha kwamba hadi kufikia Februari Mosi, 2018 upatikanaji wa mbolea nchini kwa ajili ya mahindi na tumbaku ulifikia tani 250,376 sawa na asilimia 51.6 ya wastani wa mahitaji ya tani 485,000 kwa mwaka.


“Katika kipindi hicho hicho, mbolea za kupandia na kukuzia zipatazo tani 229,839 ziliingizwa nchini na kusambazwa mikoani. Upatikanaji wa dawa za maji na unga (Salfa) kwa ajili ya mazao ya pamba na korosho unaendelea.”

Waziri Mkuu alisema hadi kufikia Februari Mosi, 2018 upatikanaji wa mbegu bora nchini ulifikia tani 51,700, sawa na asilimia 86.2 ya mahitaji halisi ya tani 60,000 kwa mwaka. Katika kipindi hicho jumla ya tani 22,357 za mbegu bora zilisambazwa nchini.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMAMOSI, FEBRUARI 10, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages