HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 11, 2018

Kijiji chakusanya milioni 800

NA SULEIMAN MSUYA

KIJIJI cha Nanjilinji A wilaya ya Kilwa mkoani Mtwara kimefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 800, kutokana na utunzaji wa misutu endelevu.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Mpingo Conservation and Development Initiative (MCDI), Jonath Timoth wakati akizungumza na Tanzania Daima ambapo alibainisha kuwa mikakati yao ni kuona wanavijiji wengi wakiongezeka katika utunzaji wa misitu.

Timoth alisema MCDI imekuwa ikishirikiana na Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) ikishirikiana kuhakikisha kuwa misitu inakuwa endelevu.
                                                                                                          
Mkurugenzi huyo alisema kiasi hicho cha fedha kimefanikisha ujenzi wa nyumba ya kulala wageni yenye vyumba 16, ofisi ya kijiji, madarasa manne na wanakikundi kunufaika kiuchumi na maendele.

Alisema mikakati yao ni kuendelea kutumia faida ambayo inapatikana kuboresha huduma za kijamii katika vijiji vilivyopo katika mradi wa utunzaji misitu pamoja na wanavijiji wenyewe.

Timoth alisema mradi wao unatekelezwa katika vijiji 40, wilaya 8 mikoa minne na matokeo yameonekana kuwa mazuri hali ambayo inawasukuma kuendelea nao.

“Tupo katika wilaya ya Tunduru ambapo kuna vijiji saba, Kilwa 10, Rufiji viwili, Liwale 15, Handeni kimoja, Namtumbo viwili, Ruangwa viwili na Nachingiwea kimoja,” anasema.

Mkurugenzi huyo wa MCDI, alisema kwa sasa wanahifadhi eneo lenye ukubwa wa hekta 410 na zaidi shilingi bilioni 1.5 zimepatikana kama mapato kwa kipindi cha miaka sita.

 “Pia wakina mama wajawazito wanapewa 100,000, watoto wakifaulu wanapewa 100,000, tunatoa bima ya afya kwa wazee, tunatoa chakula shuleni yote haya ni kuhakikisha kuwa utunzaji wa misitu unakuwa endelevu kwa kile kiinachopatikana kuwarejea watunzaji,” alisema.

Alisema pamoja na kuvuna misitu wamekuwa wakirejesha kwa kuotesha miti mingine ambapo mwaka jana waliotesha miche 4,000 ya Mkongo, mwaaka huu wanamiche 10,000 ya Mpingo na Mnungunungu 10,000 ambayo inatajwa kuwa ni miti inayopotea kwa kasi.

Timoth alisema ili kutunza misitu na kuangalia kuwa unaongezeka au unapungua wanafanya doria kila mwezi kuangalia misitu isipungue, kuangalia aina yak wanyamaa kwenye misitu na aina ya ndege ambao wanakuwepo msituni hapo.

No comments:

Post a Comment

Pages