HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 07, 2018

Sophia Kawawa kupewa tuzo ya mafanikio

NA SULEIMAN MSUYA

TAASISI ya Wanawake wenye Mafanikio Tanzania (TWA), leo itatoa tuzo ya mafanikio ya kimaisha (Lifetime Achievement Award) ya mwaka huu 2018 kwa marehemu Sophia Kawawa, kutokana na mchango wake wa kurasimisha utolewaji wa likizo zauzazi kwa wakina mama na wakina baba nchini Tanzania.

Aidha, TWA inatarajia kukutanisha wanawake viongozi zaidi ya 250 na wadau mbalimbali kuweka agenda ya kuendeleza na kuwawezesha wanawake wa Tanzania kwa pamoja na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG).

Hayo yamesemwa na Mwasisi na Rais wa TWA, Irene Kiwia wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kongamano hilo linalengo la kujenga ajenda ya pamoja ya utetezi miongoni mwa wanawake kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

Kiwia alisema marehemu Sophia amefanya mambo mengi makubwa lakini amblo linaendelea kukumbukwa na vizazi vya Tanzania ni kupigania uwepo wa likizo kwa mama na baba pale mke anapojifungua.

Alisema Sophia ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ni mwanamke wa kuigwa na kukumbukwa na jamii ya Kitanzania kutokana na kupigania mambo mbalimbali.

Aidha, alisema pamoja na utoaji wa tuzo hiyo ya mafanikio kwa Sophia pia kutakuwepo na kongamano litakaloshirikisha wanawake viongozi na wadau wengine mbalimbali.

“Katika kuazimisha siku ya wanawake duniani, TWA wamezindua kongamano la TWA forum 2018, ambalo linalenga kuwaleta pamoja viongozi wanawake kutoka kila pande ya maisha, wenye uzoefu mpana na umri tofauti kusherehekea mafanikio ya wanawake.

Alisema pia wataangazia ufumbuzi wa changamoto za uongozi wa kiuchumi ambayo yataimarisha ushiriki wa kiuchumi wa wanawake Tanzania.

Kiwia alisema wanawake wamekuwa na mchango wa kipekee katika jamii ya watanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo Sanaa na Utamaduni, Michezo, Afya, Elimu, Kilimo, Teknolojia ya Habarina Mawasiliano, Biashara na Ujasiriamali, Nyanja mbalimbali za umma, Sayansi na Teknolojia na Mafanikio ya maisha kwa ujumla.

“Kuna wanawake wengi sana Tanzania ambao wametoa mchango wao wa kipekee katika sekta mbalimbali, tunataka kutambua macho ya wanawake hawa na kusambaza habari kuhusu mafanikio yao ili kuwahamasisha wanawake wengine kuwa na malengo ya kufikia hatua hiyo na kusaidia kuongeza ubora wao,” alisema.



Kiwia alisema hatuwezi kuwa na maendeleo ya kweli sehemu yoyote pasipo kuwa na ushiriki wa kweli wa mwanamke katika sekta zote za jamii.



“Kongamano hilo litatengeneza jukwaa la kujadili changamoto mbalimbali na namna za kusuluhisha na kupata uvumbuzi ambao unaweza kuwanufaisha wanawake na hatimae kunufaisha nchi,” aliongeza.

Alisema kongomano la nusu ya mwaka la TWA linakuja katika wakati ambapo mtazamo wa ulimwengu kuhusu uwezeshwaji wawanawake unasisitizia kuhusu maendeleo katika afya na uzima, usawa katika elimu, jinsia na ushiriki wa wanawake katika uchumi miongoni mwa vitu vingine vingi.

Mwenyekiti wa TWA Sadaka Gandi alisema “Kaulimbiu ya mwaka huu ni Msukumo wa Maendeleo” na imekuja wakati ambapo dunia inamwona mwanamke anatekeleza majukumu ya msingi katika ngazi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Gandi alisema mengi yamefikiwa, lakini kuna mengi zaidi ya kukamilisha katika kuhakikisha kuwa kuna ushiriki wakikamilifu katika nyanja zote za shughuli za maendeleo.

“Tuzo zitaangazia pia uvumbuzi na jitihada kutoka kwa wanawake katika mazingira mbalimbali, ambako kila mmoja kuanzia msichana mdogo kutoka maeneo ya vijijini Tanzania mpaka mwanamke mfanyabiashara na mtengeneza sera hapa nchini na nje ya nchi, anaweza kupata hamasa kutoka kwao.” aliongeza Gandi.

Alisema katika kongamano hilo litakalofunguliwa na na Dk. Judy Dlamini, mmoja kati ya viongozi mwanamke anayeheshimiwa zaidi Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla atatumia nahasi hio kuzindua kitabu chake kipya kiitwayo“Equal But Different”.

No comments:

Post a Comment

Pages