HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 11, 2018

WAKULIMA 2000 WAONGEZA KIPATO KWA UJENZI WA DARAJA LA MIVARF

Wakulima 2000 kutoka vijiji sita vya, Kata ya Kiru Wilayani Babati wameongeza kipato kutokana na ujenzi wa daraja lililojengwa na Mradi wa Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za kifedha Vijijini (MIVARF), ikiwa ni sehemu ya malengo ya mradi huo katika kuongeza kipato nchini hususan maeneo ya vijijini.

Wakulima hao wa Kata ya Kiru, inayojumuisha kaya 306, walishindwa kuongeza kipato kwa takribani miaka 38, tangu mwaka 1978, baada ya Daraja walilokuwa wanatumia kusombwa na Mafuriko hadi mwaka 2016, Serikali kupitia Mradi wa MIVARF ilipojenga Daraja hilo ambalo limeanza kutumika sasa na kuchochea shughuli zao za kiuchumi .

Akiongea na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Mradi wa MIVARF mara baada ya kutembelea Kijiji cha Masware lilipojengwa Daraja hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Babati Hamis Malinga amesema, Serikali kupitia Mradi wa MIVARF imeweza kuchochea uwekezaji katika kata hiyo

“Kiwanda cha Sukari cha Manyara kimeweza kuongeza uzalishaji kutoka tani 15 hadi 30 kwa siku kutokana na ujenzi wa daraja la kijiji cha Masware ambalo limesaidia kuboresha biashara baina ya vijiji na kuongeza kipato kwa wananchi. Aidha, Usafirishaji wa mazao na bidhaa ulikuwa wa gharama kubwa sana lakini kwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kupitia mradi huu tumeweza kuona maendeleo makubwa katika Vijiji hivi”, alisema Mkurugenzi Malinga.

Kwa upande wa wakulima wa kijiji cha Masware wamesema ujenzi wa Daraja hilo umeongeza kipato chao kwani wanaweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi pamoja na vijana wamepata ajira kupitia usafiri wa pikipiki maarufu kama “bodaboda” unaotumiwa kusafirisha abiria

“Tangu ujenzi wa daraja hili tumeweza kupeleka mazaoyetu katika soko tunalotaka ambapo awali haikuwa rahisi, wakulima walikuwa wanalanguliwa gunia moja la mahindi lilikuwa likiuzwa kuanzia shilingi elfu 20,000 hadi 30,000 lakini kwa ujenzi wa daraja hili wananchi wanaweza kuuza mahindi kuanzia elfu 50,000 hadi 60,000 kwa gunia moja” amesema Aboubakar Mohamed.

Naye Mkulima wa Kijiji hicho Zena Mpinga ameeleza kuwa, “kabla ya ujenzi wa daraja hilo wanawake na wamama wajawazito walikuwa wakisafiri kwa shida na kwa gharama kubwa sana ambapo ukisafiri kwa kutumia pikipiki maarufu kama “bodaboda” ilikuwa ni shilingi elfu 10,000 kutokana na ukosefu wa kivuko imara na bora na kulazimu kuzunguka na pikipiki kijiji jirani ila kwa sasa usafiri wa bodaboda ni shilingi elfu 2000 hadi 3000 tu inakufikisha na kuweza kukamilisha mahitaji yako kwa wakati.

Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF), inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kutekelezwa katika Halmashauri 76 za Tanzania Bara na Zanzibar, ikiwa imegharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (IFAD) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (ADB) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

IMETOLEWA NA

KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA WAZIRI MKUU

No comments:

Post a Comment

Pages