HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 19, 2018

ANZISHENI KAMPENI ZA KUHAMASISHA UPIMAJI WA VVU-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini washirikiane na wadau wa mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kuanzisha kampeni ya kuhamasisha wananchi hususani wanaume kupima VVU na kuanza kutumia dawa mapema.

Kadhalika, amewaagiza Wakuu hao wa Mikoa na Wilaya kwa kusaidiana na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wasimamie kwa uzito unaostahili kampeni hiyo itakayoendeshwa kwa muda wa miezi sita mfululizo.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumanne, Juni 19, 2018) wakati akizindua kampeni ya Kitaifa ya kuhamasisha wananchi hususani wanaume kupima VVU na kuanza kutumia dawa mapema, iliyofanyika katika Uwanja wa Jamuhuri, jijini Dodoma.

“Kwa vile tunazindua kampeni ya kupima na kuanza ARV mara moja (Test and Treat) natoa rai kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI, mhakikishe vitendanishi na dawa za ARV zipo za kutosheleza katika kila kituo kinachotoa huduma katika kila Mkoa na Wilaya,” amesema. 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahamasisha watu wote watakaogundulika na maambukizo ya VVU waelewe kuwa utaratibu wa sasa ni kuanza dawa mara moja pasipo kujali kiwango cha kinga mwilini, yaani CD4. 

Amesema huo ni utaratibu ambao nchi imeuridhia kwa kuwa una manufaa kwa mtumiaji wa dawa na jamii kwa ujumla. “Mtu yeyote asisite kuanza dawa mara tu anapogundulika kuwa na maambukizo ya VVU bila hata kusubiri CD4 kushuka sana,”.

Katia hatua nyingine, Waziri Mkuu ametaja baadhi ya njia zitakazosaidia kuwafikia wanaume kwa ajili ya kupima VVU na kuanza dawa mara wanapogundulika kuwa na maambukizi kuwa ni pamoja na kupanua wigo wa kuwatumia wanaogundulika na maambukizi ya VVU kuwaleta wenza wao sehemu za kupata huduma.

“Kuimarisha fursa ya wahudumu wa afya kwa magonjwa mengine, kuwashawishi watumiaji wa huduma hizo kupimwa VVU, hususan wanaume na kupanua huduma za upimaji na ushauri nasaha hasa katika Mikoa na Wilaya zenye maambukizo makubwa ya VVU lakini ikiwa na watu wachache wanaojua hali zao za maambukizo,” amesema.

Pia kuainisha na kutumia maeneo ya shughuli za kiuchumi, kijamii, kidini, kimila na starehe yanayowaleta wanaume pamoja ili kuwahamasisha wanaume (wazee na vijana) kuziendea huduma za upimaji wa VVU na magonjwa mengine sugu. 

Waziri Mkuu amesema anaamini utaratibu huo utaleta matokeo chanya hasa kwa kuwatumia wanaume ambao ni viongozi na wanaoheshimika katika maeneo husika pamoja na kuziunganisha huduma za upimaji wa VVU katika upimaji na huduma za magonjwa mengine kama magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ili kuimarisha upatikanaji wa huduma katika sehemu mmoja. 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau wote wa mapambano ya VVU na UKIMWI kwamba Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais chini ya uongozi Dkt. John Magufuli, itaendelea kufanyanao kazi kwa karibu ili kwa pamoja wafikie lengo ya kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bibi Ummy Mwalimu na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Bw. Suleiman Jafo.

Wengine ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Stella Ikupa, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kuhusu Masuala ya UKIMWI, Bw. Oscar Mukasa.

Makatibu Wakuu wa Wizara, Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Dkt. Leonard Maboko, Wadau wa Maendeleo, Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Bw. Justin Mwinuka, Viongozi wa Dini na Asasi za Kiraia, Wakuu wa Mikoa na Wilaya.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMANNE, Juni 19, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages