HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 18, 2018

VIONGOZI NA WATUMISHI NCHINI WAKUMBUSHWA KUTEKELZA MAJUKUMU YAO KWA KUTANGULIZA MBELE MOYO WA UZALENDO NA MASILAHI YA TAIFA

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akiwasili katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi, jijini Dar es Salaam kufunga kozi ya siku tano ya viongozi.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akimtunuku cheti Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James baada ya kuhitimu kozi fupi ya tano ya Viongozi iliyofanyika katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi, jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza na washiriki wa kozi fupi ya tano ya Viongozi, iliyofanyika katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi, jijini Dar es Salaam.
 Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Anna Mghwira akitoa neno la shukrani baada ya kuhitimu kozi fupi ya tano ya Viongozi katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi, jijini Dar es Salaam. 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akipokea zawadi ya tai, kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Luteni Jenerali, Paul Massao, baada ya kufungua kozi fupi ya tano ya Viongozi, iliyofanyika katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi, jijini Dar es Salaam. 


Viongozi na Watumishi nchini wamekumbushwa kutanguliza mbele moyo wa uzalendo na masilahi mapana ya taifa wanapotekeleza majukumu yao ili kupeleka maendeleo ya taifa mbele na kuimarisha usalama wa taifa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wakati akifunga kozi fupi ya tano kwa viongozi iliyofanyika Chuo cha cha Taifa cha Ulinzi - Tanzania (NDC) jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mkuchika amesema, ni matumaini kuwa washiriki waliohudhuria kozi hiyo, utendaji wao wa kazi utabadilika kwa kuwa na tija kwani sasa mbinu zote zinazohusu namna ya kufikiri kimkakati, kufanya tathmini katika mambo mbalimbali ili kufikia maamuzi wamezipata.

“Sasa mnatambua dhana ya usalama wa Taifa vema na kwa mapana zaidi, si kulinda mipaka na mali za wanajamii tu, bali pia inahusisha kutunza mazingira, kuwa na chakula cha kutosha, kupiga vita rushwa na madawa ya kulevya na mengine mengi ambayo ninyi mnayafahamu zaidi,” Mhe. Mkuchika amesema na kuongeza kuwa usalama wa watu ni muhimu kuliko jambo jingine lolote, hivyo masuala ya usalama yawe ni sehemu ya kuzingatia katika utendaji wa kila siku na hasa pale maamuzi yanayogusa masilahi ya nchi na jamii yanapotolewa.

Aidha, Mhe. Mkuchika amesema, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kwa dhati kuipeleka nchi katika Uchumi wa Viwanda, lakini suala la rushwa limekuwa kikwazo kikubwa kufikia lengo hilo, hivyo ni jukumu la viongozi wote kutoa majawabu ya namna gani malengo yatafikiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi -Tanzania, Luteni Jenerali Paul Massao ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha viongozi na watumishi wengine wanahudhuria kozi hiyo muhimu kwa masilahi ya taifa.
Jumla ya wahitimu 24 walikabidhiwa vyeti, baadhi yao wakiwa ni Waheshimiwa Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi Waandamizi wa Taasisi za Serikali. 
Mtaala wa kozi hiyo ulilenga katika masuala yanayohusu masilahi, uzalendo na dhana nzima ya usalama wa taifa.
 
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 18 AGOSTI, 2018

No comments:

Post a Comment

Pages