HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 16, 2018

TAA yasaidia mafuta kinga jua kwa walemavu wa ngozi


Katibu Mkuu wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) Bw. Mussa Kabimba (aliyesimama) akizungumia changamoto wanazokutana nazo watu wenye Ualbino. Katikati ni Kaimu Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bi. Naomi Semadio na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Jeshi la Wokovu, Bw. Masoud Babu (kushoto).

Kaimu Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Bi. Naomi Semadio akitoa hotuba fupi, kabla ya zoezi la ugawaji wa mafuta kinga jua ya Ngozi kwa watoto wenye Ulemavu wa ualbino. Kulia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Jeshi la Wokovu, Bw Masoud Babu.

Kaimu Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bi. Naomi Semadio (katikati) akimkabidhi chupa ya mafuta kinga jua ya Ngozi kwa mmoja wa watoto wenye ulemavu wa Ualbino. Wengine ni Katibu Mkuu wa Chama cha Watu wenye Ulemavu Ualbino Tanzania (TAS) , Bw. Mussa Kabimba (kulia) na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Jeshi la wokovu Mwl. Masoud Babu (kushoto).


Na Mwandishi Wetu


WAKATI Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ikisaidia mafuta maalum chupa 55 ya ngozi kwa walemavu wa ngozi, imetoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia mahitaji hayo na mengine yanayowakabili.

Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Kaimu Meneja Rasilimali Watu na Utawala, Bi. Naomi Semadio, amesema Mamlaka kupitia sera yake ya kusaidia jamii (Corporate Social Responsibility Policy) imechangia mafuta kinga jua ya ngozi kwa Chama cha Watu wenye Ulemavu wa ngozi (TAS), kama sehemu ya mchango wake kwa chama hicho katika kuwajali na kuwahudumia Watanzania wenye ualbino katika kukabiliana na changamoto ya afya ya ngozi.

Semadio amesema kufuatia maombi hayo kwa kushirikiana na TAS wametoa mafuta hayo aina ya Infinity care SPF 30 Sunscreen yenye thamani ya Tshs 1,375,000 kwa watoto wa shule za msingi Uhuru Mchanganyiko na Jeshi la Wokovu (Salvation Army), lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba watoto hawa wanapata fursa ya elimu katika mazingira mazuri kwa kuhakikisha hali nzuri ya afya ya Ngozi.

« Mamlaka inatambua wajibu wake katika kuhakikisha inaboresha maisha ya watanzania, kwa kusaidia wahitaji katika jamii na inawajali watu wote wenye ulemavu bila ya kuwabagua na kwa kudhihirisha hilo imekuwa na wafanyakazi walemavu mbalimbali na wanawajali kama walivyo watu wazima wasiokuwa na ulemavu, » amesema.

Amesema moja ya msingi mkuu wa Mamlaka ni kuwajali wateja wake na wadau wake, TAA ipo kwa ajili ya kutoa huduma kwa watu wa hali zote, kwa kuzingatia hilo Mamlaka itaendelea kuwasaidia wadau wake mbalimbali wenye uhitaji.

Tayari Mamlaka imeshatoa misaada kwa watu mbalimbali ukiwemo Umoja wa Wabunge Wanawake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kujenga vyoo vya mfano vya watoto wa kike wenye ulemavu kwa majimbo yote Tanzania nzima, pia imefanikisha tamasha la Urithi Wetu lililofanyika Jijini Dar es Salaam.

Dira ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ni kuwa mtoaji wa huduma za viwanja vya ndege kwa kiwango cha Kimataifa; wakati Dhima yetu inasema Kutoa huduma bora na viwezeshi katika viwanja vya ndege kwa kuzingatia ufanisi katika matumizi ya rasilimali zilizopo.

Mamlaka inasimamia na kuendesha viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali, ambapo katika hivyo viwili ni vya Kimataifa ambavyo ni Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA).

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania inatoa shukrani kwa wadau wetu na serikali, ambapo kwa namna moja au nyingine wanamchango katika kusaidia watu wenye ulemavu.

Hatahivyo, Semadio ametoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo nchini kujitokeza kusaidia walemavu kulingana na mahitaji yao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TAS, Mussa Kabimba amesema asilimia 70 ya walemavu wa ngozi wanapoteza maisha wakiwa wadogo kutokana na kushambuliwa na ugonjwa wa saratani ya ngozi.

Kabimba amesema mazingira ya familia za wanaozaliwa na ulemavu wa ngozi, zinatokana na wakulima na wafugaji, ambapo upatikanaji wa mafuta kinga jua ya ngozi, kofia pana na miwani kwa ajili ya kuboresha afya zao ni changamoto kubwa.

«Ninaomba wadau wengine waguswe ili kutoa msaada kwa vijana wetu ili waweze kuboresha afya zao, tunawashukuru sana Mamlaka kwa namna ambavyo mlivyosaidia mafuta haya, pia nawashukuru walimu kwa kusaidia kuwaweka wanafunzi kuwa na afya nje, » amesema

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Jeshi la Wokovu (Salvation Army), Masoud Babu ameishukuru TAA kwa kusaidia wanafunzi wao, ambao sasa hawatashambuliwa na maradhi mbalimbali ikiwemo saratani ya ngozi, ambayo imekuwa ikikwamisha jitihada zao za kujiendeleza kielemu.

Akitoa neno la Shukrani mmoja wa wanafunzi, Joyce Mahona alishukuru kwa msaada huo mkubwa ambayo utawasaidia kwa kuweka ngozi zao katika afya bora, kwani awali walikuwa wakipaka mafuta ya kawaida pekee.

No comments:

Post a Comment

Pages