HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 17, 2018

Ukandamizaji unazuia wasichana kutumia simu

NA MWANDISHI WETU
KATIKA kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, ilioyofanyika Oktoba 11, Asasi isiyo ya kibiashara ya Girl Effect kwa kushirikiana na Taasisi ya Vodafone Foundation, wametoa matokeo ya utafiti wa kwanza wa kimataifa, juu uhuru kwa wasichana wadogo wanavyopata na kutumia teknolojia ya simu.

Kwa mujibu wa utafiti huo, inaonesha kwamba wavulana wana uhuru wa kuwa na simu mara 1.5 zaidi kuliko wasichana, na kuwa na uwezekano wa kuwa na simu janja (Smart phone) mara 1.3 zaidi, kutokana na  upendeleo wa kijamii na vikwazo vingine vyenye kuzuia matumizi ya simu kwa wasichana.

Akiwasilisha utafiti huo, Kecia Bertermann, ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi na Utafiti wa Kidijitali wa Girl Effect, alisema imebainika kuwa uhuru wa kutumia simu za mkononi kwa wasichana walio katika nchi zinazoendelea ni mdogo kuliko inavyotarajiwa.

Bertermann alisema ni asilimia 44 tu ya wasichana waliohojiwa katika utafiti walisema wanamiliki simu, huku zaidi ya nusu (yaani asilimia 52), wakisema hupata simu kwa kuazima kwa wenzao ambao hutumia simu hizo kwa kificho.

Aliongeza ya kwamba, utafiti huo umeonyesha kwamba asilimia 50 ya waliohojiwa walisema simu zinafanya wasichana kujisikia kutotengwa, huku asilimia 47 wakizitumia kupata elimu, asilimia 62 kwa kujiburudisha, asilimia 26 kuwafunulia habari zilizofichika na asilimia 20 kuwafanya wajiamini.

Hata hivyo, utafiti huo wa ubora na uwiano, uliofanyika katika nchi 25, umegundua kuwa uhuru wa matumizi ya simu kwa wasichana unadhibitiwa  kwa kiasi kikubwa na mazoea ya kijamii, ambayo huwazuia kuwa na uhuru sawa na wavulana.

Naye Andrew Dunnett, ambaye ni Mkurugenzi wa Vodafone Foundation, alisema wasichana wanaachwa nyuma, huku akikiri kwamba katika nchi nyingi upatikanaji wa simu ni muhimu kwa elimu, maendeleo na afya ya wasichana.

“Tunahitaji kukabiliana na ukweli kwamba wasichana na wavulana hawana uhuru sawa wa kupata simu na huduma za kiubunifu mahususi kwa ajili ya wasichana ili kukidhi mahitaji yao katika muktadha huu,” alisema Dunnett.

Aidha, Vodafone Foundation, Girl Effect wakishirikiana na wadau na washirika wengine wamedhamiria kuwawezesha wasichana milioni 7 katika nchi nane walioathirika na upatikanaji wa huduma wanazohitaji kupitia simu, kwa kukusanya fedha kiasi cha dola milioni 25 katika miaka mitano.

No comments:

Post a Comment

Pages