HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 16, 2018

UKATIKAJI WA UMEME WILAYANI MASASI MKOANI MTWARA UNAONGEZA GHARAMA ZA UENDESHAJI WA HOSPITALI YA MKOMAINDO

 Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Mussa Rashid, akizungumza na waandishi wa habari pamoja na maofisa wa Bohari ya Dawa (MSD), (hawapo pichani), wilayani humo jana, kuhusu upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi na mambo mengine.
 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Masasi Mkomaido, Selijo Kusekwa, akizungumzia upatikaji wa dawa.
 Mfamasia wa Duka la Dawa la Hospitali ya Mkomaindo, Omari Jongo (kushoto), akifurahi wakati akizungumza na waandishi kuhusu huduma za uuzaji dawa wanazozitoa kwa wateja wao. Kutoka kulia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Masasi Mkomaido, Selijo Kusekwa na Mtaalamu wa dawa, Mathias Kifaru.
 Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mkuti, Zakati Mussa (katikati) akizungumza na waandishi wa habari.

Na Dotto Mwaibale, Masasi, Mtwara

MGANGA Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Mussa Rashid amesema ukatikaji wa umeme wa mara kwa mara katika mji wa Masasi umekuwa ukiwaongezea gharama za uendeshaji wa matibabu.

Rashid aliyasema hayo wilayani humo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na maofisa wa Bohari ya Dawa (MSD) ambao wapo mkoani Mtwara kuwatembelea wateja wao ili kujua changamoto walizonazo na kuzitafutia ufumbuzi.

"Changamoto kubwa tuliyonayo ni ili suala la kukatika umeme linatuongezea gharama kubwa kwa kuwasha jenereta wakati wote kwani kama mnavyojua tunafanya upasuaji, utunzaji wa dawa na maji hivyo  bila ya umeme hatuwezi kufanya chochote hapa Hospitalini" alisema Rashid.

Mbali ya changamoto hiyo ya umeme Dkt. Rashid alisema katika miaka zaidi ya 15 aliyofanya kazi hakuna kipindi ambacho anafurahi kufanya kazi kama kipindi hiki cha awamu ya tano kinachoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwani huduma za sekta ya afya zimeboreshwa na kutengewa bajeti kubwa.

Alisema hivi sasa wakiwapokea wagonjwa wakiwasikiliza na kuchukua vipimo vya magonjwa yanayo wasumbua wanajisikia furaha na amani pale wanapoondoka wakiwa wamepata dawa na mahitaji mengine ya utabibu tofauti na zamani ambapo walikuwa wakionesha kutolizishwa na huduma zetu kwa kuwa walikuwa wakikosa dawa.

"Kwa kweli katika jambo ili nampongeza sana Rais Magufuli na kauli yake ya mara kwa mara kwetu ya kutusisitiza kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaofika kutibiwa katika hospitali zetu" alisema Dkt. Rashid.

Akizungumzia upatikaji wa dawa Dkt Rasdid alisema MSD imeboresha sana huduma zake na imekuwa ikiwapelekea dawa na vifaa tiba kwa wakati na hiyo inatokana ushirikiano mzuri uliopo baina ya MSD na hospitali hiyo.

Alisema anaupongeza uongozi wa MSD kwa kufanikisha jambo hilo kwani hivi sasa ni tofauti kabisa na miaka ya nyuma katika suala zima la ufanisi wa upatikaji wa dawa katika wilaya hiyo hivyo aliomba waendelee kuongeza juhudi ili wafikie mafanikio makubwa zaidi ya hapo.

Alisema hivi sasa wagonjwa wanalizishwa na huduma za afya wanazopata na hata wao madaktari wanafurahia hali hiyo hasa wanapowaona wagonjwa wanapata dawa baada ya vipimo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mkomaindo, Selijo Kusekwa alisema upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika hospitali hiyo ni mkubwa na wamekuwa wakizipokea kwa wakati ukilinganisha miaka ya nyuma.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mkuti iliyopo mjini humo, Zakati Mussa alisema upatikanaji wa dawa katika kituo chake ni mzuri kwani wakitoa oda MSD wamekuwa wakipelekewa kwa wakati.

Mkazi wa eneo la Jida mjini Masasi, Ahmed Ali pamoja na Nasra Omari wamesema tangu waanze kutibiwa katika Zahanati hiyo ya Mkuti hajawahi kukosa dawa hivyo wameishukuru serikali na MSD kwa kuboresha huduma za afya hasa katika upatikanaji wa dawa.

No comments:

Post a Comment

Pages