HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 19, 2019

DKT. MWANJELWA AMUONYA MWEKA HAZINA WA HALMASHAURI YA WILAYA YA KOROGWE KWA UTENDAJI USIORIDHISHA

 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Mji wa Korogwe, wakati wa kikao kazi na watumishi hao chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao kabla ya  kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Halmashauri hizo. (Picha na Ofisi ya Rais-Utumishi).
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiteta jambo na Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Bi. Zena Said, kabla ya kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Mji ya Korogwe kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao kabla ya  kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Halmashauri hizo.
Baadhi ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Mji ya Korogwe wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani), wakati wa kikao kazi chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.  

KOROGWE, TANGA

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ametoa onyo kali kwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Bw. Issai Mbilu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Fedha na Biashara wa Halmashauri hiyo kwa kutotekeleza majukumu yake ipasavyo na kumtaka kuacha kiburi na kujirekebisha mara moja ili atekeleze majukumu yake kwa kutenda haki.

Onyo hilo amelitoa wilayani Korogwe wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Mji wa Korogwe chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kabla ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kukagua miradi ya TASAF na kujiridhisha na utekelezaji wake.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amemtaka Mweka Hazina huyo, kutokuwa kikwazo kwenye malipo halali ya watumishi wenzie pamoja na kutoa sababu zenye mashiko za kukataa kuidhinisha malipo ya watumishi kwa maandishi pindi anapobaini mapungufu.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amemsisitiza Mweka Hazina huyo kuacha kuipendelea idara yake katika kulipa stahili mbalimbali ikiwamo posho ya saa za ziada kazini na kuongeza kuwa malipo ya posho hiyo sio kwa ajili ya watumishi wa Idara ya Fedha na Biashara pekee bali ni kwa ajili ya watumishi wote wa halmashauri kwani ni haki kwa mtumishi yeyote aliyefanya kazi katika muda wa ziada kulipwa stahili yake.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amefafanua kwamba,  kitendo cha kuwalipa posho ya saa za ziada watumishi wa Idara ya Fedha na Biashara pekee kinashusha morali ya utendaji kazi kwa watumishi wengine.

Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa halmashauri hizo kutofanya udanganyifu ili wapate malipo yasiyostahili kwani ni kosa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma na kusisitiza kuwa kila mtumishi afanye kazi kwa bidii ili alipwe anachostahili.

Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ametoa onyo kwa mtumishi huyo ili ajirekebishe, ikiwa ni pamoja na kutoa somo kwa watumishi wote wa umma nchini wanaofanya kazi bila kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma.

Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Tanga yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi kwa umma,  ikiwa ni pamoja na kukagua na kujiridhisha na utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.

No comments:

Post a Comment

Pages